Serikali imezindua mradi mpya wa thamani ya shilingi bilioni 21.5 sawa na dola milioni 165.5 kwa ajili ya kurejesha na kusimamia kwa njia endelevu msitu wa Mau.
Mradi huu unajulikana kama Integrated Conservation and Livelihood Improvement Programme (MCF-ICLIP), unalenga kuboresha mifumo ya ikolojia, kuinua maisha ya jamii na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika eneo la Mau.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Festus Ng’eno, ambaye pia ndiye mlezi wa mpango huu, alisema kwamba Mau ni hazina kubwa kitaifa na kikanda.
“Thamani ya huduma na rasilimali za ikolojia zinazotolewa na msitu huu inakadiriwa kufikia shilingi bilioni 197. Msitu huu unasaidia jamii zinazouzunguka na pia kuisdia mifumo ya ikolojia mashuhuri kama vile Maasai Mara na Serengeti,” alisema Dkt. Ng’eno.
Msitu huu una ukubwa wa jumla ya ekari 403,000 na unajumuisha vitalu vya misitu 22. Ni msitu mkubwa zaidi unaopatikana kwenye mlima Afrika Mashariki, wenye bioanuwai ya kipekee duniani.
Aidha, unatokana na mito mikuu 12 inayosambazia maziwa muhimu, yakiwemo Ziwa Natron ambalo ni eneo la kuzaliana ndege aina ya aina ya flamingo.
Pamoja na umuhimu wake, msitu huu unakabiliwa na changamoto kubwa zikiwemo sheria dhaifu, ukataji miti haramu, uvunaji wa mkaa, ufugaji kupita kiasi, kilimo kisicho endelevu na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hali hii imesababisha kupungua kwa misitu, uvamizi wa maeneo ya kingo za mito na uchafuzi wa maji.
Mradi huu wa miaka kumi umeundwa kwa vipengele vitano, usimamizi endelevu wa mandhari ya ikolojia, uboreshaji wa maisha ya jamii, uchumi, elimu ya mazingira na utafiti, na utawala na usimamizi wa rasilimali.
Miongoni mwa hatua kuu zitakazotekelezwa ni: kurejesha ekari 33,138 za misitu iliyoharibiwa, kukarabati mabwawa 14, kulinda chemchemi 40 na kutenga kilomita 16 za maeneo ya hifadhi ya kijamii na kiuchumi. Pia, ekari 668 za maeneo oevu na kilomita 100 za kingo za mito zitarejeshwa.
Mradi huu utafanyiwa uzinduzi rasmi Oktoba 24, katika eneo la Kuresoi Kaskazini.