Katika kitabu chake kiitwacho ‘Out of Africa’, mwandishi wa Denmark Karen Blixen aliwahi kuandika, "Nilikuwa na shamba chini ya milima ya Ngong”.
Kupitia mistari hiyo michache, mwandishi huyo alilenga kuitambulisha Kenya kwa ulimwengu.
Hili ni taifa ambalo ni kawaida kuona likizalisha vipaji kwa ajili ya mashindano ya Olimpiki na lililoanzisha teknolojia ya uhamishaji fedha ya M-Pesa na viatimizi vingine.
Hebu fikiria kuona kundi la simba karibu na barabara za Nairobi au twiga wavukao barabara.
Tofauti za kushangaza
Kenya ina ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 580,000.
Kando ya mipaka yake, taifa hilo limejaliwa vivutio mbalimbali kama vile barafu ya Mlima Kenya, fukwe za pwani na mbuga za Maasai Mara.
Taifa hili ni nyumbani kwa zaidi ya watu milioni 50, kutoka jamii mbalimbali zenye kuzungumza lahaja na lugha zipatazo 60, ikiwemo Kiswahili na Kiingereza.
Jamii hizi ni pamoja na zile za kifugaji za Wamaasai na Wasamburu.
"Tunaamini kuwa utamaduni ni kitu cha kipekee sana, hivyo hatuna budi kuupenda," anasema Joshua Ole Kaputa, mwandaaji wa wa tamasha la Kimaasai katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Urithi wa kimichezo
Wanariadha wa Kenya wamejiwekea heshima ya kipekee kwenye michezo ya Olimpiki, wakianzia kwenye barabara za vumbi hadi kwenye majukwaa ya kimataifa.
Urithi huu uliasisiwa na Kipchoge Keino baada ya kuushangaza ulimwengu kwa medali zake za dhahabu kwenye michezo ya olimpiki ya mwaka 1960 na mwaka 1970, ambazo zilitoa hamasa kwa vizazi vijavyo.
Akitajwa kama mmoja ya wanariadha wakubwa duniani, Eliud Kipchoge aliweka historia mwaka 2019 kwa kuwa mwanadamu wa kwanza kukimbia mbio za marathon chini ya saa mbili.
"Huwa tuna msemo hapa Kenya kuwa huwezi kuwakimbiza sungura wawili kwa wakati mmoja, utawakosa wote'," anasema Kipchoge. "Tuna wanariadha wengi wenye vipaji. Hatua ya kwanza ni kudhubutu, kufikiri, kuvunja na kuthubutu kulifanya hilo jambo.”
Utajiri wa kiasili
Nchi hiyo pia imejaliwa utajiri wa mali asili kama vile maajabu ya nyumbu wahamao ndani ya hifadhi ya Maasai Mara, tukio lenye kuvutia mamilioni ya watazamaji kila mwaka.
"Nimeshuhudia tukio hilo kwa mara nyingi sasa, na huwa halichoshi," anasema Maggie Reya, muongoza utalii nchini Kenya.
“Nimetembelea nchi nyingi lakini sijawahi kuona uzuri kama huu,” anasema Hashmita Shah katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Ardhi na ubunifu
Kenya ni kati ya wazalishaji wakubwa wa mazao ya chai na maua, pamoja na kahawa na bidhaa za mbogamboga na maua.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO), kilimo kinachangia asilimia zaidi ya 30 ya pato la taifa la Kenya.
Kwa sasa, Kenya ni moja ya nchi zilizopiga hatua kisiasa, kiuchumo na kidiplomasia.
Safari ya mafanikio
Safari hiyo ilianza wakati wa wapigania uhuru wa Mau Mau kwenye miaka ya 1950 na kupelekea kupatikana kwa uhuru mwaka 1963.