Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelilaani shambulizi la Israel dhidi ya hospitali ya Nasser, na kusema kuwa serikali ya Israel ya Benjamin Netanyahu inaendelea na mashambulizi yake ya kikatili kuharibu kila kitu ambacho kinachohusiana na ubinadamu bila ya kikomo.
Matamshi ya Erdogan yalikuja baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri ambao ulifanyika mashariki mwa jimbo la Bitlis siku ya Jumatatu.
Kauli yake kuhusu shambulio hilo la Israel imekuja baada ya Wizara ya Afya ya Gaza kuthibitisha kuwa Wapalestina 20 wakiwemo wagonjwa, wahudumu wa afya, walinzi wa raia na wafanyakazi wa vyombo vya habari waliuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulio hilo.
Kuhusu mradi wa korido ya Zangezur, Erdogan alisema kuwa pamoja na utekelezaji wa mradi huo pamoja na vipengele vyake vyote, ushirikiano wa kiuchumi kati ya Uturuki, Azerbaijan na Armenia utapata mwelekeo mpya.