AFRIKA
2 dk kusoma
Shirika la Amnesty International labaini ukiukwaji wa haki mashariki mwa DRC
Wapiganaji wa M23, Wazalendo, pamoja na wanajeshi wa Congol wamehusishwa na dhulma dhidi ya raia
Shirika la Amnesty International labaini ukiukwaji wa haki mashariki mwa DRC
tokea masaa 8

Siku ya Jumatano shirika la Amnesty International limeshtumu makundi yanayopigana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuhusika na dhulma, ikiwemo ubakaji, mauaji na utekaji nyara.

Katika uchunguzi wao wa hivi karibuni, shirika hilo la haki za binaadamu linasema waasi wote wa M23 na wale wa Wazalendo, kundi la wapiganaji la serikali, wamebaka wanawake na kutekeleza ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia mashariki mwa Congo.

“Ukatili wa makundi yanayopigana hauna mipaka; ukatili huu una lengo wa kuadhibu, kunyanyasa na kuwadhalalisha raia huku kila upande ukitafuta udhibiti,” alisema Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Amnesty International.

M23, inahusika katika mapigano mashariki mwa Congo, na inadhibiti maeneo mengi, ikiwemo makao makuu ya mikoa miji ya Goma na Bukavu, ambayo iliichukuwa mapema mwaka huu.

Umoja wa Mataifa, serikali ya DRC na wengine wanashtumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo la waasi, madai ambayo Rwanda inakanusha.

Hakujakuwa na taarifa yoyote kutoka kwa serikali ya DRC au waasi wa M23.

Lakini Chagutah anasema Rwanda na Congo wanatakiwa kuwawajibisha weote waliohusika na ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Shirika hilo la haki za binaadamu linasema limewahoji mashahidi zaidi ya 53, ikiwemo walioathirika na dhulma hizo, wataalamu wa afya na mashirika ya kiraia.

Shirika hilo pia lilitathmini taarifa rasmi ya M23, sauti zilorekodiwa na taarifa kutoka kwa vyombo vya habari vya maeneo hayo na kimataifa na mashirika ya haki za binaadamu.

Dhulma hizo zilifanyika mjini Goma, Bukavu, Rutshuru na Masisi pamoja na maeneo ya Kalehe, hasa kati ya mwezi wa Januari na Mei mwaka huu.

Kulingana na Amnesty International, kati ya watu 14 walionusurika unyanyasaji wa ngono ambao wamehojiwa, wanane wanasema walibakwa na wapiganaji wa M23 na watano wanasema walibakwa na wapiganaji wa Wazalendo, ilhali mmoja anasema alibakwa na wanajeshi wa Congo.

Huko Bukavu, wapiganaji watano wa M23 walimbaka mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Beatrice “katika kambi ya kijeshi ya M23,” shirika hilo lilisema.

“Kwa wanawake wa mashariki mwa DRC, hakuna palipo salama; wanabakwa majumbani mwao, katika mashamba, au kambini ambapo wanatafuta hifadhi. Dunia lazima iseme imetosha. Pande zote zinazopigana lazima zitowe kipaumbele kwa usalama wa raia, ikiwemo wanawake na wasichana ambao wanaendelea kupata matatizo makubwa ya mapigano hayo,” alisema Chagutah.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us