Wafanyakazi kadhaa wa shirika la habari lenye makao yake makuu Uingereza Reuters walizungumza katika taarifa iliyotolewa Alhamisi kuhusu kile wanachokiona kuwa upendeleo kwa Israel miongoni mwa wahariri na uongozi wa shirika hilo.
Mapema mwezi huu, kufuatia kuuawa kwa mwandishi wa Palestina Anas Al Sharif, Reuters iliandika kichwa cha habari kilosema, "Israel yamuua mwandishi wa Al Jazeera ikisema alikuwa kiongozi wa Hamas."
Kutumia vichwa vya habari vyenye utata kama hivyo vinazusha wasiwasi, hasa kwa kuwa Al Sharif zamani alikuwa mshinda wa tuzo ya Reuters' ya Pulitzer akiwa pamoja na wenzake, mtandao wa Declassified UK umeripoti.
Kichwa hicho cha habari kilisababisha malumbano mtandaoni na kuwepo kwa hali ya wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi wa Reuters, ambao baadhi yao walieleza hofu yao kisiri kuhusu kile wanachoeleza kuwa upendeleo wa Israel kuhusu maamuzi ya uhariri wa shirika hilo la habari.
Reuters, ambayo ilianzishwa jijini London in 1851 na sasa inafikia watu zaidi ya bilioni moja kwa siku, inakabiliwa na tathmini kubwa kutoka ndani.
Baadhi ya wafanyakazi wa sasa na wa zamani wa Reuters, ambao hawakutaka kutambulishwa wameiambia Declassified UK, kuhusu utamaduni wa uhariri ambao unadunisha madhila ya Palestina.
Upendeleo wa wazi
Mwezi Agosti 2024 mhariri mmoja, alieleza kuwa maadili yao hayaendani na mtazamo wa kampuni katika kuangazia taarifa za vita vya Israel Gaza.
Mhariri huyo aliweka taarifa na barua ya wazi, akitoa wito kwa uongozi kuzingatia utaratibu wa uandishi; hata hivyo, Idara ya mawasiliano ya Reuters imekanusha kupokea barua hizo.
Hata hivyo, taarifa za ndani zimethibitishia Declassified UK kuwa kufuatia vita vya Israel Gaza, kundi la waandishi wa Reuters lilifanya tathmini ya ndani ya taarifa 500 kuhusu Israel na Palestina zilizochapishwa katika kipindi cha zaidi ya wiki tano.
Uchunguzi wao ulibaini upendeleo wa wazi, huku wakiangazia zaidi mtazamo wa Israel na waliouawa upande huo, licha ya Wapalestina wengi zaidi kuuawa Gaza.
Wakati huo, Wapalestina zaidi ya 11,000 walikuwa wameuawa, ikiwa karibu mara kumi zaidi ya Waisrael waliouawa.
“Uchunguzi wa kina wa ndani, kwa kufanyia tathmini taarifa zetu”, ulifanyika, kulingana na chanzo kimoja cha Reuters, ambacho kiliwaambia Declassified UK:
“Wiki chache baada ya vita vya Israel Gaza, waandishi kadhaa wa Reuters waliona kuwa taarifa zetu za vita vya Israel na Gaza hazikuwa na mizania.”
Waandishi hao pia wameshtumu Reuters kwa kukwepa kutumia neno “Palestina” na kushindwa kuangazia madai ya wataalamu kuwa Israel inatekeleza mauaji ya halaiki, taarifa ambazo Reuters ziliripoti wazi wakati wa kuangzaia hatua za Urusi nchini Ukraine.
Licha ya shutma hizi, Reuters bado haijazungumzia suala hili hadharani kama imekubalia mapendekezo yoyote ya ndani.
Baadhi ya mabadiliko ambayo yalifanywa Mei 2024, ni kuruhusu waandishi kutumia neno “mauaji ya halaiki” kwa kutaja chanzo, lakini tathmini inaonesha kuwa neno hilo huwa halitumiki sana wakati wa kuangazia mapigano.
Tafsida
Maneno ya tafsida kama "vita’’, "kampeni", au "mashambulizi" yameshamiri, na wakati mauaji ya halaiki yakitajwa, kukanusha kwa Israel huwa kunajumuishwa, tofauti na makanusho ya makundi ya wapiganaji ya Palestina, ambayo hayapewi nafasi sawa.
Miongozi ya ndani ya shirika hilo yanaegemea sana upande wa Israel, na kuacha kabisa majukumu ya Marekani na Israel katika kukandamiza kusitishwa kwa mapigano, ulowezi wa Israel, na mazingira ya ubaguzi wa rangi ndani ya Palestina.
Muongozo huo pia hauzungumzii hali ya Gaza kama eneo baya zaidi la mzozo kwa waandishi wa habari tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani, Declassified UK imeripoti.
Wakosoaji wa vyo vya habari vya Magharibi, ikiwemo aliyekuwa mwanasheria wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Craig Mokhiber, ameshtumu mashirika kama Reuters kwa kuzuia kwa maksudi mazingira ya mauaji ya halaiki na ya kudhalilisha kwa waathiriwa wa Palestina kwa lengo la kuwalinda Waisrael wasiwajibishwe.
Mwandishi wa habari wa Israel Gideon Levy hivi karibuni alieleza kuhusu kwa waandishi kutokuwa na ujasiri wa kutoa taarifa za kweli ambazo zingeepusha kuongezeka kwa mashambulizi ya sasa ya kijeshi.
Hata hivyo, msemaji wa Reuters, alitetea taarifa za habari za shirika hilo akizitaja kuwa za “haki na zisizoegemea upande wowote”.