Nigeria imewaondoa nchini raia wa kigeni 102 ikiwemo raia wa China 50 waliopatikana na hatia ya "ugaidi wa mitandaoni na utapeli wa mitandaoni", taasisi ya kupambana na ufisadi katika taifa hilo la Afrika magharibi ilisema siku ya Alhamisi.
Raia mmoja wa Tunisia pia alikuwa miongoni mwa wale waliotimuliwa tangu Agosti 15, Taasisi hiyo ya Kupambana na ufisadi wa Kiuchumi na Fedha (EFCC) ilisema kwenye taarifa, huku wengine zaidi wakitarajiwa kuondolewa katika siku chache zijazo.
Walioondolewa nchini humo walikuwa miongoni mwa washukiwa 792 waliokamatwa katika msako wakihusishwa na wizi wa mitandaoni katika mtaa wa kifahari wa Victoria Island, jijini Lagos Disemba iliyopita.
Watu wasiopungua 192 miongoni mwa wale waliokamatwa walikuwa raia wa kigeni, Wachina wakiwa 148, EFCC ilisema.
Wanatapeli watu
EFCC ilifanikiwa kufichua maeneo mengi ambapo wahalifu vijana walikuwa wanajifunza mbinu za utapeli.
Kulingana na taasisi, magenge ya kigeni yamewajumuisha raia wa Nigeria kwenye shughuli zao hizo kutapeli watu mitandaoni, ambapo wanajaribu kuwarubuni watu kutuma fedha au kutoa taarifa zao muhimu kama vile namba zao za siri.
Matapeli hao wanawalenga zaidi raia wa Marekani, Canada, Mexico na Ulaya.
Wataalamu pia wanaonya kuwa "wizi wa mitandaoni" wa raia wa kigeni wanafanya shughuli zao nchini humo kutokana na mifumo dhaifu ya kukabiliana na usalama wa mitandaoni.