Watu wa Palestina wanahitaji "hatua yetu ya pamoja," Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alisema Jumatatu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu (OIC) kuhusu Gaza.
Akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Mataifa ya Kiislamu (OIC) uliofanyika katika mji wa Jeddah nchini Saudi Arabia, mwenyekiti wa mkutano huo Fidan alisema, "Wanachohitaji watu wa Palestina ni hatua yetu ya pamoja".
Ameonya kuwa utambuzi wa taifa la Palestina hautoshi bila hatua ya kimataifa kuilazimisha Israel kukomesha vita vyake.
"Serikali ya Israel haitaki amani bali kufutwa kwa Palestina. Hili haliwezi kuruhusiwa," alisema.
"Lazima wakomeshwe."
Mkutano wa OIC, unaoongozwa na mwanadiplomasia mkuu wa Uturuki, unaangazia hatua zinazoendelea za Israel huko Gaza na unalenga kuratibu misimamo na majibu ya nchi wanachama.
Katika hotuba ya ufunguzi, Fidan pia alilaani mashambulizi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, wakiwemo mawaziri wa Israel, akisisitiza kwamba vitendo hivyo haviwezi kuendelea bila kudhibitiwa katika mji huo wa kihistoria.
Israel imewauwa karibu Wapalestina 62,700 katika hujuma ya kikatili huko Gaza tangu Oktoba 2023.
Vita hivyo vimeharibu eneo hilo, ambalo linakabiliwa na njaa iliyosababishwa kimakusudi na Israeli.
Makubaliano ya Gaza
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Uturuki alisisitiza umuhimu wa pendekezo la kusitisha mapigano kati ya Misri na Qatar, ambalo linaweza kusaidia kusitisha mashambulizi ya Israel, akibainisha kuwa OIC itaunga mkono kikamilifu juhudi za kusitisha mapigano Gaza.
"Mkataba unafikiwa, lakini mchokozi [Israeli] lazima pia akubali," Hakan Fidan alisema.
Fidan alionya kwamba kushindwa kupata usitishaji mapigano kutaruhusu kuendelea kukaliwa kwa mabavu na ukatili, akihimiza mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuwa mwanachama kamili wa Palestina.
Alisisitiza mipango ya ujenzi na ukarabati wa Gaza lazima ifuate mfumo wa Kiarabu na Kiislamu, huku Uturuki ikijitolea kikamilifu kuunga mkono juhudi hizo.
"Lazima tuhakikishe kwamba Wapalestina wanasalia Gaza. Ni lazima tuujenge upya Ukanda wa Gaza pamoja," Fidan alisema.
Fidan alikumbusha kwamba OIC ilianzishwa kulinda Msikiti wa Al Aqsa, akisema udhaifu wowote ungedhoofisha misheni ya msingi ya shirika hilo.
Pia alitahadharisha kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria, Lebanon na Iran yanaakisi ajenda pana ya uvunjifu wa amani ambayo inatishia usalama wa kikanda na kimataifa.