Siku ya Jumatatu Israel ilisema itatuma msaada Sudan Kusini, huku Israel ikiendelea kuwa pingamizi kwa Ukanda wa Gaza ambapo imeacha watu wakiwa katika baa la njaa.
Katika taarifa iliyotolewa na Redio ya Jeshi, Wizara ya Mambo ya Nje inasema Israel itatoa msaada wa dharura kwa Sudan Kusini kufuatia mlipuko wa kipindupindu ambao umeenea tangu Septemba 2024.
Chombo cha habari cha umma cha Israel KAN kinasema tangazo hilo linakuja “huku kukiwa na ripoti za majadiliano na Sudan Kusini kuhusu kuwapeleka wakazi wa Gaza kwenye eneo hilo,” Ingawa serikali ya Sudan Kusini ilikanusha kuwepo kwa makubaliano hayo.
Kulingana na gazeti hilo Israel Hayom, msaada huo, unaosimamiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Gideon Saar, utajumuisha dawa, vifaa vya kusafisha maji, na vyakula.
Tangazo hilo limeshtua watu kwa sababu Israel imefunga mpaka wa kuingia Gaza tangu Machi 2, ikizuia kupita kwa msafara wa misaada na kuruhusu tu kiasi kidogo ambacho hakitoshi kusaidia watu.
Mashirika ya haki za binaadamu na maafisa wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakishtumu Israel kwa kutumia njaa kama silaha katika vita dhidi ya watu wa Gaza.
Mwezi uliopita, Saar alikuwa mwenyeji wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini Mundi Samaia Kumba mjini Jerusalem, akimshkuru kwa namna nchi yake inavyounga mkono Israel. Wakati wa ziara hiyo, Kumba alitembelea makazi ya walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Vyombo vya habari vya nje viliripoti mapema mwezi huu kuwa Sudan Kusini imeidhinisha kuwapokea watu wa Palestina watakaoondolewa Gaza kwa lengo la kupata uwekezaji kutoka Israel. Sudan Kusini baadaye ilikanusha madai hayo, ikiyaita “yasiyokuwa na msingi.”
Siku ya Jumatatu, shirika la Amnesty International limeshtumu Israel kwa kusababisha “kwa maksudi njaa” huko Gaza na “kumaliza kabisa maisha na afya ya watu wa Palestina.”
Israel imewaua Wapalestina zaidi ya 61,900 Gaza tangu Oktoba 2023. Jeshi limeharibu eneo hilo na kusababisha njaa kali.
Novemba iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya ICC ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu Gaza.
Israel pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa vita vyake katika eneo hilo.