Marekani imetangaza masharti mapya ya viza kwa raia wa Nigeria, yanayohitaji waombaji wote kuweka wazi akaunti zao za mitandao ya kijamii katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa lengo la kufanyiwa mchujo.
‘‘Kutoweka taarifa za mitandao ya kijamii kunaweza kusababisha mtu kunyimwa viza na uwezekano wa kukosa viza katika siku za baadaye,’’ Ubalozi wa Marekani nchini Nigeria ulisema katika taarifa kwenye mtandao wa X siku ya Jumatatu, ukiongeza kuwa wanaotuma maombi ya viza ‘‘wanahitaji kuweka wazi akaunti zao za mitandao yote ya kijamii ambayo wametumia katika kipindi cha miaka 5 iliyopita katika fomu ya maombi ya DS-160.’’
Serikali ya Nigeria bado haijasema lolote kuhusu taarifa hii mpya ya viza za Marekani.
Agizo hili linakuja huku ikiweka masharti makali ya viza zake na kuweka vikwazo vya usafiri kwa nchi kote duniani, hasa kwa mataifa ya Afrika.
Mwezi Julai, Nigeria iliiomba serikali ya Trump kufikiria upya kuhusu vikwazo vya muda uliowekewa raia wake wa Nigeria wa kukaa nchini humo kwa muda usiozidi miezi mitatu. Masharti hayo yameathiri pia mataifa ya Cameroon na Ethiopia.