Serikali ya Uganda imeafikiana na Marekani makubaliano ya kuwapokea na kuwapa hifadhi wahamiaji walionyimwa kuingia Marekani.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Uganda Bagiire Vincent Waiswa, mpango huo utahusisha kuwapokea wahamiaji wenye rekodi za uhalifu, watoto wasio na walezi, na wale wanaosita kurudi makwao.
Waiswa aliongeza kuwa, nchi hizo ziko mbioni kukamilisha mpango na makubaliano hayo.
Hatua hiyo inakuja licha ya kuwepo na madai ya awali kuwa Uganda haikuwa tayari kuwapokea wahamiaji hao.
“Ninavyoelewa mimi, bado hatujafikia makubaliano hayo,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Henry Okello Oryem siku ya Jumatano.
Hadi kufikia sasa, ni Sudan Kusini, Rwanda na Eswatini yaliyokubali kupokea wahamiaji waliorudishwa kutoka Marekani.