Kadi ya mpira wa kikapu inayowahusisha magwiji wa NBA, Michael Jordan na Kobe Bryant, iliuzwa kwa rekodi ya dunia ya dola milioni 12.932 katika mnada uliofanyika katika jimbo la Texas, Marekani. Hii imekuwa kadi ya michezo ghali zaidi kuwahi kuuzwa.
Heritage Auctions, kampuni ya mnada iliyoko Dallas, ilitangaza kupitia jukwaa la kampuni ya mitandao ya kijamii ya Marekani, X, Jumapili kwamba kadi hiyo ya 2007-08 Upper Deck Exquisite Collection Dual Logoman Autographs ilivunja rekodi wakati wa mnada wa Summer Platinum Night Sports uliofanyika Jumamosi.
"Dau kwa ajili ya kadi ya 2007-08 Upper Deck Exquisite Collection Dual Logoman Autographs Michael Jordan & Kobe Bryant #DL-KM Signed ilipanda juu kama wachezaji waliopo kwenye kadi hiyo hadi kufikia dola milioni 12.932," ilisema kampuni ya mnada.
Kadi hiyo ina sifa ya kipekee kwa kuwa na picha, saini, na vipande vya nembo za jezi za NBA za magwiji hao wawili wa mpira wa kikapu. Ni kadi pekee ya Dual Logoman inayowahusisha Jordan na Bryant, ambapo kipande cha jezi ya Jordan ni toleo maalum la dhahabu.
Muamala huu ulivuka rekodi ya awali ya kadi ya NBA ya dola milioni 5.2 kwa zaidi ya mara mbili na pia ulipita kwa kiasi kidogo rekodi ya mnada wa kadi ya michezo iliyowekwa na kadi ya 1952 Topps Mickey Mantle ambayo iliuza kwa dola milioni 12.6 mwaka 2022.
Kadi ya Jordan-Bryant sasa inashikilia nafasi ya pili kwa thamani kubwa zaidi ya kumbukumbu za michezo katika historia, ikitanguliwa tu na jezi ya Babe Ruth ya World Series ya mwaka 1932, ambayo iliuza kwa dola milioni 24.12 mwaka 2024.
Jina la mnunuzi wa kadi hiyo halijafichuliwa.
Jordan anachukuliwa na wengi kama mchezaji bora zaidi wa NBA kuwahi kutokea, akiwa ameshinda mataji sita, huku Bryant, gwiji mwingine wa mpira wa kikapu, akishinda mataji matano kabla ya kifo chake cha ghafla Januari 2020 katika ajali ya helikopta.