Licha ya kutawaliwa na vita kwa wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu sasa, taifa la Sudan limeshangaza watu wengi barani Afrika, baada ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya CHAN 2024.
Sudan imefanikiwa kufanya hivyo baada ya kuitoa miamba mingine ya soka barani Afrika, Algeria kwa mikwaju ya penati 4-2 na hivyo kujiandaa kumenyana na Madagascar siku ya Jumanne.
Licha ya mafanikio hayo, je, unafahamu kwamba nchi hiyo imeshindwa kuendesha ligi zake za ndani kutokana na machafuko ya kisiasa.
Mwaka 2024, klabu ya Al Hilal ya Sudan ililiomba Shirikisho la Soka Nchini (TFF), kuiruhusu timu hiyo kushiriki Ligi Kuu nchini Tanzania, kutokana na sababu za kiusalama.
Kwa sasa, timu kubwa za Sudan kama vile Al-Mereikh, Al Hilal na Al Khartoum hucheza michezo yao ya Ligi nchini Libya na mara nyingine Sudan Kusini.
Ili kuwaweka fiti wachezaji wao wa ndani, Sudan pia imeruhusiwa kushiriki ligi kuu ya nchini Mauritania.
Kwa upande wa udhamini wa ligi, fedha za kuendesha ligi yao mara nyingi hutolewa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na watu wa Saudia Arabia.