AFRIKA
1 dk kusoma
CHAN 2024: Tanzania kuvunja mwiko wa kufungwa na Morocco?
Timu ya taifa ya Tanzania, maarufu kama ‘Taifa Stars’, inajitupa uwanjani Agosti 22, 2025, kukabiliana na Morocco, katika mchezo wa robo fainali ya CHAN 2024.
CHAN 2024: Tanzania kuvunja mwiko wa kufungwa na Morocco?
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania./@Tanfootball / Others
tokea masaa 20

Macho na masikio ya Watanzania wote kwa sasa, yapo katika timu ya taifa ya nchi hiyo, maarufu kama ‘Taifa Stars’, itakapokuwa inasaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya CHAN 2024.

Kikosi cha Tanzania, kinachoongozwa na Hemed Suleiman Ali, maarufu kama kama ‘Morocco’, kitashuka kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kujaribu kuwapa furaha Watanzania, wanaposaka nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo maalumu kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani.

‘Taifa Stars’, ambayo ilimaliza kundi B ikiwa na alama 10, na kushika nafasi ya kwanza, imekuwa na matokeo mabaya dhidi ya Morocco kwenye michuano ya kimataifa.

Katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, mchezo uliofanyika Machi 26, 2025, Tanzania ilikubali kufungwa mabao 2-0 na Morocco, iliyokuwa na akina Brahim Diaz wa Real Madrid na Achraf Hakimi wa PSG.

Januari 14, 2024, Morocco iliifunga Tanzania mabao 3-0, katika michuano ya AFCON, iliyokuwa ikifanyika nchini Ivory Coast.

Mara ya mwisho Tanzania kuifunga Morocco, ilikuwa ni mwaka 2013, katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia.

Ikiongozwa na Mdenmark Kim Poulsen, ‘Taifa Stars’ ilishinda mabao 3-0, yakitiwa kimiani na Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us