Spika wa zamani wa bunge la Nigeria ambaye baadaye alikuwa gavana wa jimbo la Sokoto amekamatwa na Tume ya kupambana na ufisadi wa Kiuchumi na Fedha (EFCC) kuhusu madai ya ufisadi
Aminu Tambuwal alikamatwa Jumatatu katika makao makuu ya tume jijini, Abuja, kuhusiana na ubadhirifu wa fedha karibu Naira bilioni 189 (milioni $123).
Haifahamiki kama nafasi zake za zamani zina uhusiano wowote na madai hayo. Tambuwal mwenye umri wa miaka 59 alikuwa bado anahojiwa Jumatatu jioni na hajazungumzi wazi kuhusu madai hayo.
Madai ya kutoa pesa hizo yanaaminika ni ukiukwaji wa sheria ya Kutakatisha Fedha ya 2022, vyombo vya habari vya Nigeria vimeripoti.
Tambuwal alikuwa spika wa Baraza la Wawakilishi kati ya 2011 na 2015 na baadaye kuwa gavana wa jimbo la Sokoto kuanzia 2015 hadi 2023. Sasa hivi ni seneta wa Sokoto Kusini.
Ni mmoja wa viongozi wa upinzani anayeunga mkono muungano wa upinzani, ADC, unaolenga kumuondoa madarakani Rais Bola Tinubu katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Msemaji wa Tume ya Kupambana na Ufisadi, Dele Oyewale, hakutaka kuzungumzia kukamatwa kwa Bwana Tambuwal.