Vyama mbalimbali vya kisiasa nchini Tanzania vinaendelea kuchukua fomu za wagombea wa kiti cha urais pamoja na makamu wake.
Miongoni mwa wagombea urais waliokabidhiwa fomu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania za kugombea kiti cha urais na makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Agosti 11, 2025, ni George Gabriel Bussungu kupitia tiketi ya Chama cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA).
Bussugu aliambatana na mgombea wake mwenza, Ali Makame Issa.
Kwa mujibu wa kalenda ya INEC, dirisha la kuchukua fomu hizo kwa nafasi ya uraia litakamilika Agosti 27.
Mgombea wa chama tawala CCM ambae pia ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mgombea wake mwenza, tayari wamechukua fomu Agosti 9, 2025.
Zoezi la uteuzi linatakiwa kukamilika Agosti 27 ambayo ndio siku ya uteuzi kwa wagombea kiti cha urais na makamu, ubunge na udiwani.
Ingawa tayari shamrashamra za kampeni zimeanza katika baadhi ya vyama, Agosti 28, 2025 ndio itakuwa siku rasmi ya kuanza kwa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.