Kenya imeshuhudia moja ya wikiendi mbaya zaidi mwaka huu, kufuatia msururu wa ajali zilizoshuhudiwa nchini humo.
Chirchir alisema Wizara yake imezindua "ukaguzi wa usalama" nchini kote na ukaguzi katika sehemu za barabara zinazokabiliwa na ajali ili kubaini hatari, kujenga upya barabara kwenye maeneo ya ajali, na kuja na mapendekezo ya kiufundi ndani ya siku saba.
Waziri huyo aliongeza kuwa mageuzi ya sheria yako katika hatua ya juu zaidi ili kuimarisha sheria za usalama barabarani haswa katika usafiri wa shule, uendeshaji wa magari ya biashara, madereva walevi, ukaguzi wa magari, vituo vya kando ya barabara, na mapitio ya Sheria ya usalama barabarani.
Waziri huyo vile vile amesema Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) itaongeza kampeni ya kutoa elimu kwa umma ili kuhimiza matumizi salama ya barabara.
“Nawaomba wadau wote wa usafiri, waendeshaji na watumiaji wa barabara, wakiwemo madereva, wanaotembea kwa miguu, bodaboda na waendesha baiskeli, kuweka kipaumbele usalama wao na kuzingatia kwa makini miongozo ya usalama barabarani,” alisema Waziri huyo.
"Ajali za barabarani zinatabirika na pia zinaweza kuepukika iwapo watumiaji wote wa barabara watatekeleza wajibu wao."
Mojawapo ya ajali mbaya zaidi wikiendi hii ilikuwa katika barabara kuu ya Kisumu-Kakamega Ijumaa jioni, wakati basi la shule lililokuwa likisafirisha waombolezaji kutoka Nyahera hadi Nyakach katika Kaunti ya Kisumu lilipopinduka katika eneo la kona la Coptic, na kuua watu 26.