Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema kuwa sekta ya ulinzi ya Uturuki, ambayo ni chanzo cha fahari kwa taifa, "inaandika halisi historia." Ameyasema haya katika toleo la baharini la tamasha kubwa la teknolojia la Uturuki, TEKNOFEST, lilopewa jina la ‘Blue Homeland’.
Tamasha hilo la siku nne linafanyika katika Makao ya Jeshi la Meli ya Istanbul. Ingawa lilianza rasmi siku ya Alhamisi, umma utaruhusiwa kuhudhuria kuanzia Agosti 29 hadi 31.
Erdogan amesema kuwa wakati marafiki wa Uturuki wanapongeza mafanikio yake, mahasimu wake wanahangaika kujaribu kuyafikia.
Ameongeza kuwa kama vile harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo zilivyowapa matumaini watu waliodhulumiwa miaka 100 iliyopita, sasa hivi juhudi katika sekta ya ulinzi zinawatia moyo wanyonge na waliokandamizwa.
“Popote pale ambapo kuna ndugu anayeteseka — kutoka Palestina hadi Syria, kutoka Yemen hadi Somalia, kutoka Sudan hadi Libya — wanajivunia mafanikio ya Uturuki,” amesema.
Erdogan amesema kuwa katika muda mfupi tu, Uturuki imefikia kiwango kinachoonewa wivu na mataifa mengine duniani.
Ameeleza pia kuwa Uturuki inaendelea kuimarisha sekta yake ya ulinzi sambamba na kuongeza hamasa kwa kizazi kipya katika masuala ya teknolojia, kidigitali, na ubunifu.
Ameongeza kuwa wageni wa tamasha hilo watapata nafasi ya kuona maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika teknolojia ya kijeshi ya baharini ya Uturuki.