Sherehe kuu ya teknolojia, na anga za juu ya Uturuki, iitwayo Teknofest, imefungua toleo maalum la baharini jijini Istanbul, likiangazia nguvu ya kijeshi ya majini ya nchi hiyo pamoja na ubunifu wa kisasa.
Tukio hilo la siku nne, linalojulikana kama ‘Blue Homeland’ taifa la buluu, lilianza siku ya Alhamisi katika Kituo cha Jeshi la Meli cha Istanbul.
Shirika la habari la Anadolu ni mshirika rasmi wa mawasiliano wa kimataifa wa hafla hiyo. Ingawa tamasha lilianza rasmi Alhamisi, umma utaruhusiwa kuhudhuria tarehe 30 na 31 Agosti.
Rais Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kushiriki katika siku ya ufunguzi.
Mashindano ni sehemu kuu ya tukio hilo, yakiwemo mashindano ya mifumo isiyo na rubani ya chini ya maji, makombora ya chini ya maji na vyombo vya baharini visivyo na rubani.
Jeshi la Wanamaji la Uturuki pia litaonesha baadhi ya meli zake za hali ya juu, kama vile:
Meli ya kushambulia ya TCG Anadolu, meli ya kivita ya Frigate ya TCG Istanbul, Korveti ya kupambana na manowari ya TCG Burgazada, meli ya Frigate ya TCG Orucreis, meli ya kuweka mabomu ya baharini TCG Nusret, pamoja na manowari za TCG Sakarya na TCG Hizirreis.
Mbali na teknolojia ya kijeshi, ‘Teknofest Blue Homeland’ pia inatoa maonesho ya historia na utamaduni wa baharini, uzoefu wa mwingiliano kupitia mfumo wa (VR- virtual reality) - teknolojia inayomruhusu mtu kuingia kwenye mazingira ya kidijitali, na mfululizo wa mikutano na kongamano.
Baada ya tukio hili, toleo kuu la Teknofest litafanyika Septemba 17–21 katika Uwanja wa Ndege wa Ataturk, Istanbul.