UTURUKI
2 dk kusoma
Uturuki iko tayari kusaidia mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi, Erdogan amwambia Zelenskyy
Erdogan amesisitiza kuwa Uturuki inaendelea na juhudi zake kuhakikisha kuwa vita vya Ukraine vinamalizika kwa amani ya kudumu.
Uturuki iko tayari kusaidia mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi, Erdogan amwambia Zelenskyy
Erdogan amueleza Zelenskyy ya kuwa kwa kupatikana kwa amani, Uturuki itaendelea kuchangia katika usalama wa Ukraine. / / AA
tokea masaa 18

Marais wa Uturuki na Ukraine wamejadili uhusiano wa pande mbili, mchakato wa amani kati ya Ukraine na Urusi, pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa kupitia mazungumzo ya simu.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amemfahamisha mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, kwamba Ankara inafuatilia kwa karibu mawasiliano yanayoendelea huko Alaska na Washington, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Alhamisi kwenye jukwaa la kijamii la NSosyal na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki.

Mazungumzo hayo yalifanyika saa chache baada ya shambulio la Urusi mjini Kiev lililosababisha vifo vya raia wasiopungua 14, wakiwemo watoto, na kuathiri maeneo ya makazi pamoja na miundombinu ya kiraia, jambo lililozua shutuma kali kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya na washirika wa Magharibi.

Erdogan “alisisitiza kuwa Uturuki inaendelea na juhudi zake kuhakikisha kuwa vita vinaisha kwa amani ya kudumu,” taarifa ilisema.

Aidha, “alieleza kuwa suluhisho la haki kwa vita vya Ukraine na Urusi linawezekana, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mazungumzo kati ya pande zote mbili, na akaonesha utayari wa Uturuki kufanya kila iwezalo kuwezesha mawasiliano ya ngazi ya juu ambayo yatafungua njia ya amani.”

Pia alieleza kuwa kwa kupatikana kwa amani, Uturuki itaendelea kuchangia katika usalama wa Ukraine.

Erdogan pia alimpongeza Ukraine kwa kuadhimisha Siku ya Uhuru wakati wa mazungumzo hayo ya simu, kwa mujibu wa taarifa ya kurugenzi.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us