AFRIKA
2 dk kusoma
Chama cha upinzani Tanzania CHAUMMA, kimezindua rasmi Jumapili Kampeni yake ya Urais
Katika hotuba yake, mgombea Urais Salum Mwalimu alizungumzia uwezeshaji wa watu mashinani, na kupendekeza uingiliaji kati wa moja kwa moja kama kufufua uchumi wa ndani na viwanda vya enzi za ukoloni.
Chama cha upinzani Tanzania CHAUMMA, kimezindua rasmi Jumapili Kampeni yake ya Urais
CHAUMMA Tanzania kimezindua rasmi kampeni yake ya urais, Kinondni jijini Dar es Salaam / CHAUMMA / TRT Afrika Swahili
tokea masaa 15

Vyama vya upinzani CHAUMMA na CUF Jumapili wamezindua rasmi kampeni zao za urais leo, ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi harakati zao kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania.

Uzinduzi wa kampeni ya leo ulijumuisha taarifa kwa umma kuthibitisha dhamira ya CHAUMMA ya kuongeza furaha miongoni mwa Watanzania, kupunguza ukosefu wa ajira, na kufufua sekta za kiuchumi kama pamba na viwanda.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo katika viwanja vya Biafra, Kinondoni jijini Daresalaam, mgombea wa urais wa chama hicho Salum Mwalimu alisisitiza lengo lake la kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu kwa kufuata maono ya muda mrefu ya mwanzilishi Hashim Rungwe.

‘‘Uchaguzi huu wa 2025, sio uchaguzi wa kawaida, ni uchaguzi wa maamuzi magumu. Ni uchaguzi wa kuamua kuendelea na hisoria ya maumivu, ahadi hewa na umasikini,’’ alisema Mwalimu. ‘‘ Au tunaanza ukurasa mpya wa maendeleo ambao kwa miaka 63 ya uhuru, serikali zote za CCM zimeshindwa kutumia fursa za rasli mali nyingi kuleta maendeleo.’’ aliongezea.

Mkutano huo ulisisitiza uwezeshaji wa watu mashinani, na kupendekeza uingiliaji kati wa moja kwa moja kama kufufua uchumi wa ndani na viwanda vya enzi za ukoloni, kando na maendeleo ya miundombinu ili kukuza ukuaji shirikishi.

Katika hotuba yake, Mwalimu , ambaye alitaja taaluma yake pamoja na ya mgombea mwenza wake Devotha Minja kama waandishi wa habari, aliahidi kuwa serikali yake itainua sekta ya uanahabari kama mhimili serikali.

‘‘Kwasababu ya imani thabiti niliyonayo juu ya tasnia ya habari, nafasi, mchango na umuhimu wake katika maendeleo ya taifa lolote, tukiingia madarakani tutaifanya habari sio tu kuwa sekta bali kuwa mhimili kama ilivyo serkali, bunge na mahakama.’’ alisema Mwalimu.

CHAUMMA iliyoanzishwa mwaka 2013 chini ya uongozi wa Hashim Rungwe Spunda inalenga kuainisha upya uwepo wake katika jukwaa la kitaifa.

Mwenyekiti wa chama, Rungwe, aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na anaendelea kutetea sera kama vile umoja wa kitaifa, uwajibikaji wa serikali, kufufua uchumi, na kutokomeza umaskini.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us