Tume hiyo ya IEBC ilieleza kuwa itaanza mchakato wa usajili Septemba 29, huku maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 yakipamba moto.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, Tume imesema inalenga kupata wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18, na raia wa Kenya ambao hawakuwa wamejisajili awali, pamoja na wale wanaotaka kuhamisha vituo vya kupiga kura.
Kulingana na Mwenyekiti wa IEBC Erastus Edung Ethekon, mchakato huo ni kwa mujibu wa kifungu 88(4) cha Katiba ya Kenya, 2010, inayotaka Tume kuendeleza usajili wa wapiga kura wakati wote.
"Mchakato huu ni hatua ya kuhakikisha kuwa kila Mkenya ambaye ametimiza umri wa kupiga kura anapata fursa hiyo ya kushiriki katika kufanya maamuzi ya mustakabali wa nchi yake kupitia uchaguzi wa kidemokrasia," Ethekon alieleza.