Uturuki siku ya Jumatano ililaani na kukataa matamshi yaliyotolewa na waziri mkuu wa Israel kuhusu matukio ya 1915.
"Tamko la (Benjamin) Netanyahu kuhusu matukio ya 1915 ni jaribio la kutumia matukio mabaya ya zamani kwa sababu za kisiasa," Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika taarifa.
"Netanyahu, ambaye anatakiwa mahakamani kwa kuhusika katika mauaji ya halaiki yaliyofanywa dhidi ya watu wa Palestina, anajaribu kuficha uhalifu ambao yeye na serikali yake wamefanya," ilisema wizara hiyo.
"Tunalaani na kukataa taarifa hio, ambayo haiendani na ukweli wa kihistoria na kisheria," iliongeza.
Uturuki inapinga uwasilishaji wa matukio kama "mauaji ya halaiki," ikiyaelezea kama janga ambapo pande zote mbili zilipata hasara.
Ankara imependekeza mara kwa mara kuundwa kwa tume ya pamoja ya wanahistoria kutoka Uturuki na Armenia, pamoja na wataalam wa kimataifa, ili kukabiliana na suala hilo.
Israel imewauwa karibu Wapalestina 63,000 huko Gaza tangu Oktoba 2023. Mashambulizi ya kijeshi yameharibu eneo hilo ambalo linakabiliwa na njaa, na kusababisha kutokuwa na makazi.
Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.
Israel pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa vita vyake dhidi ya Gaza.