Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema "siku itakuja ambapo hatimaye ndugu na dada zetu wa Palestina, ambao wanalengwa kwa risasi na mabomu mbele ya kamera kila siku, wataona haki ikitendeka."
Akizungumza katika hafla ya kuhitimu Chuo cha Walinzi wa Pwani na Askari wa Usalama wa Ndani jijini Ankara siku ya Jumatano, Erdogan alisema: “Wale wanaomwaga damu ya wasio na hatia, nao pia wataangamia katika damu hiyo hiyo."
Matamshi ya Erdogan yalitolewa saa chache baada ya Spika wa Bunge la Uturuki, Numan Kurtulmus, kuitisha kikao maalum cha Bunge siku ya Ijumaa kujadili mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, pamoja na mauaji ya halaiki, ukandamizaji na sera za kusabibisha njaa.
Ofisi ya Spika ilitangaza siku ya Jumatano kuwa Kurtulmus aliikitisha kikao hicho maalum kwa mujibu wa Kifungu cha 93 cha Katiba na Kifungu cha 7 cha Kanuni za Bunge.
Hapo awali, Rais Erdogan alikuwa amelaani shambulio la Israel dhidi ya Hospitali ya Nasser, akiituhumu serikali ya Netanyahu kwa “kuendelea kuangamiza ubinadamu bila huruma,” baada ya maafisa wa Gaza kusema kuwa watu 20 waliuawa, wakiwemo wagonjwa, wahudumu wa afya, wafanyakazi wa uokoaji na waandishi wa habari.
Tangu Oktoba 2023, Israel imewaua takribani Wapalestina 63,000 huko Gaza.
Vikwazo vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, vilivyowekwa tangu mapema mwezi Machi, vimesababisha hali mbaya ya kibinadamu kwa wakazi wake milioni 2.4, ikiwa ni pamoja na baa la njaa, kuenea kwa magonjwa, na kusambaratika kwa huduma muhimu.
Mwezi Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Waziri wa zamani wa Ulinzi, Yoav Gallant, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Gaza.
Aidha, Israel inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutokana na vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza.