AFRIKA
2 dk kusoma
Rwanda yapokea wahamiaji waliotimuliwa kutoka Marekani mapema mwezi huu
Rwanda imepokea wahamiaji saba waliotimuliwa kutoka Marekani mapema mwezi huu, msemaji wa serikali alisema kupitia taarifa siku ya Alhamisi, wiki chache baada ya nchi hizo mbili kufikia makubaliano ya kuhamisha hadi watu 250.
Rwanda yapokea wahamiaji waliotimuliwa kutoka Marekani mapema mwezi huu
Serikali ya Rwanda imeahidi kuwapatia wahamiaji hao msaada wa huduma za kijamii, afya, mafunzo ya kazi na makazi. / / Reuters
tokea masaa 10

“Kundi la kwanza la wahamiaji saba waliokaguliwa liliwasili Rwanda katikati ya mwezi Agosti,” alisema Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya Rwanda, katika taarifa hiyo.

“Watu watatu kati yao wameonesha nia ya kurejea katika nchi zao za asili, huku wanne wameamua kubaki na kujenga maisha yao nchini Rwanda. Bila kujali mahitaji yao binafsi, watu hawa wote watapatiwa msaada unaofaa na ulinzi kutoka kwa serikali ya Rwanda.”

Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani hazikutoa majibu mara moja zilipotafutwa kuhusiana na suala hili.

Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa na msimamo mkali kuhusu uhamiaji, akilenga kuwatimua mamilioni ya wahamiaji walioko nchini humo kinyume cha sheria na kuongeza juhudi za kuwaondoa kwa kuwatuma katika nchi zingine.

Mapema mwezi Agosti, Rwanda na Marekani zilikubaliana na Rwanda kupokea hadi wahamiaji 250, huku Washington ikituma orodha ya awali ya watu 10 kwa ajili ya ukaguzi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Rwanda imejitangaza kama nchi inayowakaribisha wahamiaji wanaotakiwa kuondolewa na mataifa ya Magharibi, licha ya wasiwasi wa mashirika ya haki za binadamu kuwa Kigali haitii umuhimu wa kutosha katika kuheshimu haki za msingi za binadamu.

Utawala wa Trump unasema kwamba kuwatuma wahamiaji katika nchi zingine kunasaidia kuwaondoa haraka baadhi ya wahamiaji, wakiwemo wale waliopatikana na hatia ya makosa ya jinai.

Wanaounga mkono hatua hiyo wanaiona kama njia ya kukabiliana na wahalifu ambao ni vigumu kuwarejesha kwao na wanaoweza kuwa tishio kwa usalama wa umma.

Wapinzani wa mpango huo wameukosoa vikali wakisema ni wa hatari na wa kikatili, kwani wahamiaji wanaweza kutumwa katika nchi ambazo wanaweza kukumbana na ghasia, hawana uhusiano wowote nazo, wala hawawezi kuzungumza lugha ya huko.

Makolo alisema mapema mwezi huu kuwa chini ya makubaliano hayo na Marekani, wahamiaji watakaotimuliwa hadi Rwanda watapatiwa mafunzo ya kazi, huduma za afya, na makazi.

Alhamisi hii, tarehe 28 Agosti, Makolo alisema kuwa wahamiaji hao waliokuwa wakihamishwa hadi Rwanda waliandamana na shirika la kimataifa na wanapokea pia msaada kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na huduma za kijamii za Rwanda.

CHANZO:Reuters
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us