AFRIKA
2 dk kusoma
Kampeni zang'oa nanga Tanzania, upinzani hauonekani
Kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania, zimeanza rasmi. Kitakuwa ni kipindi cha panda shuka kwa vyama vya siasa nchini humo ambapo kila chama kitakuwa kinanadi sera zake ili kupata ridhaa ya wananchi
Kampeni zang'oa nanga Tanzania, upinzani hauonekani
Tanzania kampeni / TRT Afrika Swahili
tokea masaa 11

Kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania, zimeanza rasmi. Bila shaka kitakuwa ni kipindi cha panda shuka kwa vyama vya siasa nchini humo ambapo kila chama kitakuwa kinanadi sera zake ili kupata ridhaa ya wananchi.


Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania, jumla ya vyama 18 vinashiriki katika mchakato huo wa kikatiba, ambapo kati ya hivyo, ni vyama 17 ambavyo vimesimamisha mgombea urais, hii ni baada ya mgombea urais kupitia chama cha upinzani ACT Wazalendo kuenguliwa dakika ya mwisho. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini humo, imedai uteuzi wa Luhaga Mpina ndani ya ACT Wazalendo ulikiuka taratibu.

Hatua hiyo, imelaaniwa na wengi, wakidai ni njia ya kufinya demokrasia na ofisi hiyo kutumika vibaya kwa lengo la kutotoa fursa sawa kwa vyama vya upinzani.
Punde tu baada ya Tume ya Huru ya Uchaguzi kutangaza kuanza rasmi kwa kipindi cha miezi miwili cha kampeni, mpaka sasa ni chama tawala CCM pekee ndicho kilichoonekana kuzindua rasmi kampeni yake.

Uzinduzi huo, ulifanyika rasmi katika viwanja wa Tanganyika Packers vilivyopo katika eneo la Kawe, jijini Dar es Salaam, ambapo maelfu walifurika katika uzinduzi huo.


Akinadi sera zake mbele ya hadhira hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan ambae, ndie anayepeperusha bendera ya CCM aliainisha vipaumbele vyake iwapo atapata ridhaa ya wananchi ya kuwa rais wa nchi hiyo kwa awamu nyengine.


“Katika siku 100 za uongozi wangu, nitahakikisha nimeunda tume maalumu ya maridhiano na upatanishi,” alisema Rais Samia.

Leo ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa kampeni hizo. Upande wa upinzani, bado kunaonekana kimya, kwani mpaka sasa, hakuna chama ambacho kimezindua rasmi kampeni yake.

Kwa upande wa wadadisi wa masuala ya siasa, baadhi walionekana kuhoji miezi miwili iliyotengwa ya kampeni na kusema, ni michache hasa ikizingitiwa kwamba, Tanzania ni nchi kubwa ambayo sio rahisi kufikika ndani ya muda huo.

Kwa upinzani, kuchelewa kuzindua kampeni zao, kunaibua maswali kadhaa, moja wapo, ni iwapo wako tayari kwa mchakamchaka unaowakabili?

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us