SIASA
2 dk kusoma
Sudan yasitisha kununua bidhaa kutoka Kenya kwa sababu ya RSF
Hatua hii inakuja baada ya Kenya kuruhusu kikosi cha RSF kuunda serikali mbadala ya Sudan katika ardhi yake.
Sudan yasitisha kununua bidhaa kutoka Kenya kwa sababu ya RSF
Kenya imesema inatafuta suluhu ya kuleta amani Sudan. / Reuters
14 Machi 2025

Sudan ilitangaza siku ya Alhamisi kuwa inapiga marufuku uagizaji bidhaa zote kutoka Kenya baada ya nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mikutano ya vikosi vya RSF na washirika wao. Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Biashara na Ugavi wa Sudan Omar Ahmed Mohamed Ali, Shirika rasmi la Habari la Sudan (SUNA) liliripoti.

Kulingana na amri hiyo, kusimamishwa kwa uagizaji bidhaa "kunatokana na Uamuzi wa Baraza la Mawaziri Nambari 129 ya 2024, ambao unasimamisha uagizaji wote kutoka Kenya kupitia bandari zote, vivuko vya mpaka, viwanja vya ndege na maeneo ya kuingilia."

Taarifa ya mawaziri ilihalalisha marufuku hiyo kama jibu kwa Kenya kuwa mwenyeji na kufadhili shughuli na mikutano ya RSF, ikisema kuwa hatua hiyo ilikuwa muhimu kulinda maslahi ya taifa na usalama wa Sudan. Marufuku itaendelea kutekelezwa hadi ilani nyingine.

Maagizo hayo yanaagiza "mamlaka zote zinazohusika kutekeleza marufuku hiyo mara moja." Serikali ya Kenya haijatoa jibu. Sudan inaagiza bidhaa kadhaa kutoka Kenya ikiwa ni pamoja na chai, vyakula na bidhaa za kutengenezea dawa.

RSF pamoja na makundi ya kisiasa na makundi yenye silaha ya Sudan, walitia saini mkataba wa kisiasa Februari 22 nchini Kenya ili kuunda serikali mbadala inayopinga mamlaka ya Sudan. Serikali ya Sudan ilipinga hatua ya Kenya kuandaa "njama ya kuanzisha serikali" kwa RSF.

Mgogoro wa kibinadamu

Mnamo Februari 20, Sudan ilimwita nyumbani balozi wake nchini Kenya, Kamal Jabara, kupinga kuhusika kwa Kenya katika majadiliano yenye lengo la kuunda "serikali mbadala."

Wanajeshi wa Sudan na RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023 katika vita ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na wengine milioni 14 kuwa wakimbizi, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Utafiti kutoka vyuo vikuu vya Marekani, hata hivyo, unakadiria idadi ya vifo kuwa karibu 130,000.

Jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa inaendela kutoa wito wa kusitishwa kwa vita, ikionya juu ya hali mbaya kwa raia huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us