Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF wamekabidhi dozi milioni 1.1 ya chanjo ya kipindupindu kwa serikali ya Chad siku ya Alhamisi, amesema afisa mmoja nchini humo.
Chanjo hizo zinatarajiwa kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati huku idadi ya vifo ikiongezeka.
Mlipuko wa kipindupindu, maambukizi ya bakteria yanayosababishwa na unywaji wa maji au ulaji wa chakula kichafu, ulitangazwa rasmi Julai 13 na umesababisha vifo vya watu 75 mashariki mwa Chad, kulingana na takwimu zilizotolewa Jumatano na maafisa wa afya.
Mahamat Hamit Ahmat, Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Afya, aliwaambia waandishi wa habari kuwa chanjo hizo zitasaidia kupambana na mlipuko wa kipindupindu katika majimbo ya Sila na Ouaddai na kuzuia maambukizi mapya.
Ahmat alisema kampeni ya chanjo itafanyika kuanzia Septemba 2 hadi 8 katika wilaya tano za afya mashariki mwa nchi hiyo.
Ugonjwa unaoenea haraka
Kipindupindu kimeenea katika mataifa kadhaa ya Afrika ikiwemo Sudan, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hali iliyochochewa na mafuriko yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) na Shirika la Afya Duniani siku ya Jumanne walizindua mpango wa dharura wa maandalizi na mwitikio wa kipindupindu kwa bara la Afrika kwa kipindi cha Septemba 2025 hadi Februari 2026.
Mashirika hayo yalisema mpango huo unalenga kufanikisha uhamasishaji wa rasilimali za ndani kwa haraka ili kufadhili chanjo na vifaa vya usimamizi wa maambukizi ya kipindupindu ili kupambana na milipuko ya sasa.
Hii itasaidia nchi 54 wanachama wa bara hilo kupunguza vifo vya kipindupindu kwa asilimia 90 na kutokomeza kipindupindu katika angalau nchi 20 ifikapo mwaka 2030.
Mpango wa kipindupindu
Hakainde Hichilema, bingwa wa kimataifa na wa bara la Afrika wa kipindupindu wa Umoja wa Afrika (AU) na rais wa Zambia, alizindua mpango huo, akisema kutokomeza kipindupindu barani Afrika si lengo la kiafya pekee bali pia ni wajibu wa kimaadili, kichocheo cha ukuaji wa uchumi, na hatua muhimu kuelekea kufanikisha Ajenda ya AU ya 2063.
"Ili kufanikiwa, lazima tuchukue hatua leo kwa ajili ya kesho bora, tukijenga Afrika inayojitegemea inayozalisha chanjo zake na kujihakikishia mustakabali wake," alisema Hichilema.
Kumekuwa na ongezeko la kutisha la maambukizi ya kipindupindu barani, likiathiri nchi 23. Angalau maambukizi 213,586 na vifo 4,507 vimeripotiwa mwaka 2025 pekee, jambo linaloonyesha umuhimu kwa kuwepo mwitikio wa haraka, alisema Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC Jean Kaseya.