Katiba imesaidia vipi kuimarisha demokrasia nchini Kenya?
AFRIKA
5 dk kusoma
Katiba imesaidia vipi kuimarisha demokrasia nchini Kenya?Kenya leo inaadhimisha miaka 15 tangu katiba mpya kuanzia kufanya kazi nchini humo. Licha ya haki ya kikatiba ya kujieleza, waandamanaji wa Gen Z nchini humo wamejikuta matatani na vyombo vya usalama waliotumia nguvu kupita kiasi.
Vijana wa GenZ walioandamana Kenya / Reuters
27 Agosti 2025

Go back! Go Back!!. Ni kauli ya hasira aliyotolewa na kijana mmoja dhidi ya polisi waliokuwa wamejihami na silaha wakati wa mojawapo ya maandamano nchini Kenya.

Tangu kuzuka kwa maandamano ya Gen Z mwaka mmoja na miezi kadhaa sasa, kumekuwa na video za kusisimua aghalabu nyengine zikiwashangaza wengi, kuona ujasiri walioonesha vijana hao pindi walipokuwa wakikabiliana na polisi wa kutuliza ghasia.

Binti mmoja alionekana akivutana na polisi na kutaka kumvua barakoa aliyovaa. Huku kijana mwingine akionekana kuwakimbiza polisi kwa panga licha ya kurushiwa mabomu ya kutoa machozi.

Kama hakungekuwa na video mtandaoni kuonyesha haya matukio, wengi wangefikiria ni simulizi ya paukwa pakawa.

Katiba ya Kenya ya 2010 iko wazi juu ya uhuru wa kujieleza

Lakini yaliyotokea wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z yalikuwa ni kuelezea malalamiko yao mengi dhidi ya serikali ikiwemo, ubadhirifu wa fedha za umma, deni kubwa la serikali, nyongeza ya kodi, utekaji wa wanaharakati na mengine mengi.

Ili kuelewa vijana wa Gen Z wameutoa wapi ujasiri huu, inabidi kurudi nyuma takriban miaka kumi na tano iliyopita, wakati wa kupitishwa kwa katiba mpya.

Na ni dhahiri kwamba, ni katiba hiyo mpya ndiyo iliyowapa kinga waandamanaji ya kutoka barabarani na kukabiliana na polisi.

‘‘Katiba lazima ieleweke kama hati inayotoa/kuweka masharti ya kanuni na dhana ambazo hazitekelezeki kivyake katika hati yenyewe,’’ anasema Edward Ndonga, mwanasheria kutoka Kenya.

‘‘Hata hivyo, katiba ya Kenya ya 2010 iko wazi juu ya uhuru wa kujieleza, sio tu inataka usawa lakini inathamini umuhimu wa 'sisi wananchi' katika utawala bora na uzingatiaji wa katiba,’’ Ndonga ameiambia TRT Afrika.

Hatari ya vyombo vya usalama

Mchakato ulikuwa mgumu na wa muda mrefu, ambao hatimaye uliwasilishwa kwa Wakenya walioupitisha katika kura ya maoni kwa asilimia 67. Hii ina maana kuwa yaliyomo yalifikiriwa katika ngazi zote za kitaifa na kuidhinishwa na wengi, kwa hiyo uelewa wake unatarajiwa kuwa mkubwa.

Suala la iwapo haki zimethibitishwa ndani ya katiba sio la kujadiliwa. Haki nyingi zimo hata hii ya kujieleza, kukusanyika na kuandamana.

‘‘Ni katika kutekeleza kwa kikamilifu ndipo kitumbua huingia mchanga. Utawala uliopo mara nyingi hujaribu kugeuza dhana hiyo kwa uhalali wa kisiasa au kufunika sauti zinazopingana na kutoa wito wa uwazi na uwajibikaji kama historia ya hivi majuzi ilivyoonyesha,’’ Ndonga ameiambia TRT Afrika.

Licha ya kujinadi kwa mwamvuli wa haki ya kikatiba ya kujieleza, vijana wengi walijikuta matatani na vyombo vya usalama.

Msimamo usiotetereka

Taswira za kutisha za vijana wa Gen Z wakipigwa marungu au hata kupigwa risasi peupe, zilitilia shaka nguvu ya uhuru huu wa kujieleza.

Madai ya vijana wengi kutekwa na kutoweka kwa sababu ya misimamo yao dhidi ya utawala, na matamshi yao kukashifu serikali kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, yalisababisha mshtuko sio tu miongoni mwa Wakenya lakini pia jamii ya kimataifa.

‘‘Mara ya kwanza mimi kwenda katika maandamano ilikuwa Juni 25 2024, wakati wa kupinga mswada wa sheria ya fedha,’’ anasema Irene Wambui, mmoja wa waandamanaji.‘‘ Mwanzoni unaingiwa na hofu hujui kama utarudi salama. Lakini mwishowe unahisi fahari fulani kwamba umeshiriki katika kitu muhimu na umechangia sauti yako,’’ anaiambia TRT Afrika.

Licha ya hayo, pamoja na vitisho vingi, vijana wa Gen Z walionekana kutoterereka, na badala yake, walijitokeza kwa wingi zaidi katika maandamano yaliyofuata.

‘‘Utekelezaji wa sheria unakusudiwa kutoa ulinzi sio tu kwa waandamanaji lakini pia kuwajibika na kazi yao ya ulinzi kwa wengine wote, licha ya maandamano. Katika hili, ninaamini kwamba utekelezaji wa sheria umeshindwa na wameamua kutumia vibaya mamlaka zao,’’ anasema Ndonga.

Kukamatwa kwa ‘wachochezi’ wa maandamano

Ajabu ni kuwa uvunjaji huu wa sheria au kwa kiasi upindaji wake kwa maslahi ya utawala umekubalika au kufumbiwa macho na serikali mbali mbali.

‘‘Utawala uliopo mara nyingi hujaribu kugeuza dhana hiyo kwa uhalali wa kisiasa au kubana sauti zinazowapinga na kutoa wito wa uwazi na uwajibikaji kama taswira ya hivi majuzi inavyodhihirisha,’’ anaongeza Ndonga. ‘‘Inatosha kusema kwamba uhuru wa kujieleza sio haki inayoweza kudharauliwa.’’ Ndonga anaambia TRT Afrika.

Na hili limeonekana katika nguvu kupita kiasi wanayotumia polisi kudhibiti maandamano.

‘‘Sisi hatukwenda barabarani kutafuta kupigwa, ni hao polisi ambao mara nyingi wanaanza fujo na kutushambulia kwa mabomu ya kutoa machozi, na kuvuruga kila kitu,’’ anasema Irene.

Wakati maandamano ya Kenya yakishika kasi chini ya uongozi wa Gen Z, kwengine barani Afrika kulichipuka ari kwa vijana wao pia kuamka na kuelezea malalamiko yao japo kupitia maandamano ya mtandaoni.

Nchi kadhaa zilijaribu kuiga wito huo, kama Nigeria, Uganda au hata Zimbabwe. Lakini maandamano hayo yalizimwa hata kabla ya kuanza huku serikali zao zikiweka ulinzi mkali na kuwakamata walioonekana kuchochea maandamano.

Uelewa wa katiba

Hii ilidhihirisha utofauti kati ya sheria na uelewa wa katiba kati ya nchi hizi. Sio kila mmoja anajua haki zake.

Basi hawa vijana wa Gen Z wa Kenya wanaelewa kweli katiba yao kwa upana wanaojipigia kifua?

‘‘Jibu fupi na tamu ni, ndio, kuna ufahamu zaidi wa haki za watu na kelele kubwa kutoka kwa kizazi kipya ambacho kimeelimika zaidi na kinaweza kupata na kusambaza habari haraka kuliko hapo awali,’’ anasema mwanasheria Ndonga.

Irene anasema utumiaji wa mtandao umewasaidia zaidi kusoma katiba na kuweza kujadiliana.

‘‘Mimi na marafiki zangu tunajadiliana kwa upana mambo yanayotuhusu katika katiba na kama hutukuelewa kuna makundi mengi mitandaoni ya wasomi wa sheria wako tayari kujibu masuali na kutufahamisha. Tukiingia barabarani ni kuwa tunajua ni haki yetu, na tunaelewa tunayokwenda kudai,’’ Irene anaambia TRT Afrika.

Yote tisa, kilichobainika wazi kutokana na maandamano ya vijana wa Kenya, ni kuwa hawaogopi tena kupaza sauti zao pindi wanapokuwa wamekwazika. Wanajikinga na haki yao kikatiba. Lakini ni kiasi gani watapewa uhuru huo na serikali, ni suala la kujadiliwa kutoka utawala mmoja hadi mwingine.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us