Kampuni ya dawa la Novartis ilisema Jumanne ilipokea idhini nchini Uswizi kwa Coartem Baby, ambayo ilisema ilikuwa dawa ya kwanza ya kutibu malaria kwa watoto wachanga na watoto wadogo.
Nchi nane za Afrika zilizoshiriki tathmini hiyo sasa zinatarajiwa kutoa idhini ya haraka ya matibabu hayo ambayo pia yanajulikana kwa jina la Riamet Baby katika baadhi ya nchi.
Novartis ilizindua Coartem ya kutibu malaria mwaka 1999, na dozi mpya sasa iliyoundwa kwa ajili ya watoto wadogo.
Matibabu hayo yameandaliwa kwa msaada wa kisayansi na kifedha kutoka kwa Shirika lisilo la kiserikali la Medicines for Malaria Venture (MMV) la Uswizi linalofanya kazi ya kusambaza dawa za kutibu, kuzuia na kutokomeza ugonjwa unaoenezwa na mbu.
Toleo hili jipya la watoto wachanga la Coartem linaweza kuyeyushwa, kuchanganywa katika maziwa ya mama, na lina ladha tamu ya matunda.
“Hadi sasa, hakujawa na matibabu ya malaria yaliyoidhinishwa kwa watoto wachanga wenye uzito wa chini ya kilo 4.5 (pauni 9.9), na kuacha pengo la matibabu,” Novartis alisema.
Kwa sasa matibabu ya malaria yanayopatikana yamejaribiwa kwa watoto wenye umri wa miezi sita pekee, kwa sababu watoto wadogo zaidi kwa kawaida hawajumuishwi katika majaribio ya matibabu.
Hapo awali, watoto wachanga wametumia mchanganyiko wa dawa uliokusudiwa kwa watoto wakubwa, na kuongeza hatari ya kupokea dawa iliyokuwa na nguvu zaidi. Na chanjo za malaria pia zilikua hazijaidhinishwa kwa watoto wachanga zaidi.
Nchi nane zilizoshiriki tathmini hiyo ni Burkina Faso, Côte d'Ivoire, Kenya, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Tanzania na Uganda.
“Takriban watoto milioni 30 huzaliwa katika maeneo yenye hatari ya malaria barani Afrika kila mwaka, huku uchunguzi mmoja kote Afrika Magharibi ukiripoti maambukizi kati ya asilimia 3.4 na asilimia 18.4 kwa watoto wachanga walio na umri wa chini ya miezi sita,” Novartis ilisema.
Dawa hizo zitasambazwa kwa kiasi kikubwa na sio kwa msingi ya kupata faida, Novartis ilisema.
"Pamoja na washirika wetu, tunajivunia kuwa tumeenda mbali zaidi kuendeleza matibabu ya kwanza ya malaria yaliyothibitishwa kwa watoto wachanga na watoto wadogo, kuhakikisha hata wale walio katika mazingira magumu zaidi wanaweza kupata huduma wanayostahili," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Novartis Vas Narasimhan.