Idadi ya vyama vya siasa vilivyochukua fomu za kugombea nafasi ya Urais na Makamu wa Rais katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, utakaofanyika Oktoba 29, 2025, imefikia 11.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), jumla ya vyama vya siasa 14 vinatarajiwa kuchukua fomu hizo, zoezi lililoanza Agosti 9, 2025.
Hata hivyo, hadi kufikia Agosti 12, jumla ya vyama vya siasa 11 vilikuwa vimechukua fomu za kuwania nafasi ya Urais na Makamu wa Rais, katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
Vyama hivyo ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Chama Cha Kijamii (CCK), Chama cha MAKINI, United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National League for Democracy.
Vingine ni National Reconstruction Alliance(NRA), Tanzania Labor Party (TLP), Union for Multiparty Democracy (UMD), Tanzania Democratic Alliance (TADEA) na Alliance for African Farmers Party (AAFP).
Ikumbukwe kwamba, chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA hakitoshiriki uchaguzi wa Oktoba 2025 baada ya kushindwa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, wakitaka kufanyike kwa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini humo.
Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Tanzania Bara zinatarajiwa kuanza Agosti 28, 2025 na kumalizika Oktoba 28, mwaka huu, huku kwa upande wa Zanzibar, kampeni zitaanza Agosti 28, 2025 na kumalizika Oktoba 27, kulingana na INEC.
Wakati huo huo, idadi ya majimbo kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2025 yatakuwa 272 kutokana na ongezeko la majimbo mapya manane yaliyotangazwa leo ambapo 222 yakiwa Tanzania Bara huku 50 yakiwa Tanzania Zanzibar, huku idadi ya wanaume waliojiandikisha kupiga kura ikiwa ni milioni 18.7 na wanawake wakiwa ni milioni 18.9.
INEC imesema kuwa tayari wapigakura 37,655,559 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu 2025.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 26.55 kutoka milioni 29.7 waliokuwa wamejiandikisha katika daftari mwaka 2020.