Mwanamuziki wa Nigeria, Davido, na mchumba wake Chioma Rowland wamefanya harusi ya kifahari katika jiji la Miami, Marekani.
Kwa mujibu wa Davido, tukio hilo lililofanyika Jumapili, Agosti 10, liligharimu dola milioni 3.7 za Kimarekani kuandaliwa.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na watu mashuhuri wa Nigeria, wakiwemo tajiri mkubwa barani Afrika, Aliko Dangote, gavana wa jimbo la Abia lililoko kusini mashariki mwa Nigeria — Alex Otti, na mjomba wa Davido, Ademola Adeleke, ambaye ni gavana wa jimbo la Osun lililoko kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Wengine waliokuwepo ni aliyekuwa Rais wa Seneti ya Nigeria, Bukola Saraki, mwanamuziki wa injili wa Marekani, Kirk Franklin, wasanii wa Nigeria Adenkule Gold na D'banj, pamoja na Stonebwoy kutoka Ghana.
Harusi ya tatu
Davido alimwambia Chioma kwamba licha ya kutumbuiza kwenye majukwaa mengi duniani, sherehe ya Miami ilikuwa "hofu kubwa zaidi."
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 32 alimuelezea Chioma, mwenye umri wa miaka 30, kama "upendo wake, amani yake, na makazi yake," akiongeza kwamba Chioma aliingia katika maisha yake "kimya kimya na kuwa sehemu yenye sauti kubwa na ya kupendeza zaidi."
Hii ni sherehe ya tatu ya harusi kwa wanandoa hao baada ya kubadilishana viapo mbele ya mahakama jijini Lagos, Nigeria, Machi 2023, na harusi ya kitamaduni pia jijini Lagos, Juni 2024.
Katika mahojiano ya awali, Davido alisema alikutana na Chioma kabla ya kuwa maarufu sana. Wawili hao walikutana katika Chuo Kikuu cha Babcock kilichopo jimbo la Ogun, kusini magharibi mwa Nigeria, mwaka 2013.
‘Kila kitu isipokuwa mke’
Davido alikuwa akisomea shahada ya muziki, huku Chioma akisomea shahada ya uchumi katika chuo hicho. Baadaye, Chioma alionyesha nia ya kuwa mpishi wa kitaalamu wa kibinafsi.
Wakati Davido na Chioma walipokutana kwa mara ya kwanza, wimbo wa Davido "Dami Duro" ulikuwa ukitamba kwenye redio, na taaluma yake ya muziki ilikuwa ikianza kupaa.
Katika mahojiano ya awali, Davido alisema mmoja wa marafiki zake wa karibu mara nyingi alimcheka akisema kwamba alikuwa na kila kitu maishani isipokuwa mke.
Msanii huyo aliongeza kuwa anashukuru kwamba alikutana na Chioma kabla ya kuwa maarufu. Kwa maneno yake, Davido alisema: "Kama ningekuwa mseja leo, na nikakutana na mwanamke, ningehisi labda ananizungumzia kwa sababu mimi ni Davido, mtu maarufu mwenye pesa."
Tukio la kusitikisha zaidi'
Licha ya kuwa kwenye uhusiano kwa miaka mingi, Davido alimtangaza Chioma hadharani kama mpenzi wake kwa mara ya kwanza mwaka 2018.
Wanandoa hao walipata mtoto wa kiume mnamo Oktoba 2019. Hata hivyo, mtoto huyo, Ifeanyi Adeleke, alifariki kwa kuzama kwenye bwawa la kuogelea akiwa na umri wa miaka mitatu mnamo Oktoba 2022, katika tukio la kusikitisha nyumbani kwa Davido jijini Lagos.
Mnamo Oktoba 2023, Chioma alijifungua mapacha.