Waliwahi kubezwa kuwa wavivu, wategemezi wa mitandao ya kijamii, na wasiojali siasa. Lakini leo, kizazi cha Gen Z nchini Kenya, kimejidhihirisha kuwa nguvu mpya ya mabadiliko — kikiongoza harakati kubwa za kupinga serikali, kuzua mjadala wa kitaifa, na kuamsha ari ya kizalendo kote nchini.
Maandamano yaliyosababishwa na kupinga Mswada wa Fedha 2024 yameweka historia. Kwa mara ya kwanza katika enzi ya kidijitali, vijana wa umri wa miaka kati ya 16 hadi 26 walijikusanya kwa njia ya mitandao ya kijamii, wakapanga, wakatekeleza, na hatimaye kumshurutisha Rais William Ruto kuondoa mswada huo bungeni.
“Sisi hatungoji. Tunaleta mageuzi sasa hivi,” alisema Anita Barasa maarufu kama Anini, binti wa miaka 17 aliyetoa wito kupitia jukwaa la TikTok, na kusambaa kwa zaidi ya mara 500,000.
Maandamano yaliyoratibiwa mitandaoni
Tofauti na harakati za zamani zilizoongozwa na wanasiasa au wanaharakati maarufu, maandamano haya yalikuwa ya kizazi kipya: hayakuwa na kiongozi rasmi, hayakufadhiliwa, na hayakuzingatia vyama vya siasa.
Badala yake, majukwaa kama TikTok, Instagram, na X (zamani Twitter) yaligeuzwa kuwa vituo vya kutoa elimu za uraia, kurusha matangazo ya moja kwa moja, na kuratibu mikutano.
“Tulitumia TikTok kuelimisha watu kuhusu mswada, siyo tu kupinga, bali kueleza kwanini unatuathiri,” alisema Zaha Indimuli, mshiriki wa maandamano kutoka Nairobi.
Maandamano hayo yaliungwa mkono na mamilioni ya Wakenya, ndani na nje ya nchi. Maeneo zaidi ya 26 yalishuhudia maandamano, huku vijana wakijitokeza kwa wingi kuandamana kwa amani licha ya vitisho vya polisi.
Hasira za kizazi kilichopuuzwa
Vijana wengi wa Gen Z wanakabiliwa na ukosefu wa ajira, gharama kubwa ya maisha, ukosefu wa fursa, na mzigo wa madeni ya taifa usiowahusu moja kwa moja.
“Hatuwezi kubeba mizigo yenu milele. Tumefika mwisho,” aliandika mmoja wa wanaharakati mtandaoni.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za kibinadamu, watu wapatao 36 walipoteza maisha mwezi Julai 2025, huku jeshi la polisi nchini humo, likituhumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
Picha za vijana waliouawa au kukamatwa zilizunguka mitandaoni na kuibua hasira zaidi.
Sauti ya vizazi vingine
Ingawa Gen Z walikuwa msitari wa mbele, walipata uungwaji mkono kutoka kwa vizazi vingine.
Milenia — watu wa miaka 27 hadi 42, walishiriki maandamano na mijadala mitandaoni, wakiwa na kauli moja: “Tumevumilia vya kutosha.”
“Hatupigi kelele tu. Tunaandaa kizazi cha viongozi wapya,” aliandika Boniface Mwangi, mwanaharakati maarufu aliyeshiriki maandamano hayo.
Viongozi wa serikali walionekana kushindwa kukabiliana na mtindo huu mpya wa uanaharakati.
Mbunge maarufu Oscar Sudi alidai kuwa vijana hawajausoma mswada huo; mshauri wa rais, David Ndii, alitaja uanaharakati wa kidijitali kama "masturbation ya kisiasa".
Kauli hizo zilionekana kama dharau kwa kizazi kilicho tayari kufa kwa ajili ya kesho yao.
“Hatuna viongozi wanaosikiliza. Lakini sasa tuna nguvu ya kuwasukuma,” alisema Fatma Noor, mwanafunzi wa chuo kikuu aliyeandamana Mombasa.
Je, Ni mwisho au mwanzo mpya?
Tayari Gen Z wameapa kwamba maandamano ni mwanzo tu. Wanajipanga kwa uchaguzi wa 2027 kwa kusajili wapiga kura, kuanzisha mijadala ya sera, na hata kugombea nafasi mbalimbali.
“Hatupigi kelele tu. Tunaandaa kizazi cha viongozi wapya,” aliandika Boniface Mwangi, mwanaharakati maarufu aliyeshiriki maandamano hayo.
Nao vinogozi mbali mbali wa upinzani wameanza kuwashawishi vijana wa Gen Z kujisajili kama wapiga kura na kujiunga na vyama vyao.
Naibu Rais wa Kenya aliyeondolewa madarakani, Rigathi Gachagua, ni miongoni mwa waliotoa wito kwa vijana hao kujiunga na upinzani.
Gachagua alisema, “Natoa wito kwa vijana wa kizazi cha Gen Z kusitisha maandamano, kuwa na utulivu na badala yake kuchukua vitambulisho, kujisajili kama wapiga kura na kujiunga na chama cha upinzani.” Akieleza hiyo ndio njia ya kumtoa Rais wa Kenya William Ruto madarakani.
Gachagua ameendelea kusema watoto wanauliwa ovyo ovyo na awaonea huruma sana na hakuna haja ya kuuliwa kwa sababu nchi ya Kenya bado inawahitaji.
Aidha baadhi ya vijana waliokuwa mstari wa mbele wakati wa maandamano ya kwanza ya kupinga mswada wa fedha wamejiunga na vyama mbali mbali.