Unapolitaja taifa la Cameroon, basi kumbukumbu za haraka zinazokujia kichwani ni majina kama Roger Mila, Thomas N'Kono na Samuel Eto'o.
Ndiyo, hawa ni magwiji waliong’ara na klabu mbalimbali ulimwenguni na pia kuifanya Cameroon iheshimike kisoka barani Afrika.
Lakini kuna zaidi ya hayo kuhusu nchi ya Cameroon.
Je, unajua kuwa Cameroon ni moja ya nchi zenye viongozi wenye umri mkubwa Afrika?
Ukiacha Paul Biya, ambaye ndiye rais wa nchi hiyo, mwenye umri wa miaka 92, akiwa tayari ametawala taifa hilo kuanzia Novemba 6, 1982, yupo mtu anaitwa Marcel Niat Njifenji.
Akiiongoza seneti ya nchi hiyo, katika nyadhifa ya urais wa chombo hicho, Njifenji ana umri wa miaka 90.
Kabla ya kuwa rais wa seneti, mhandisi huyo wa zamani, amewahi kuwa mkurugenzi wa taasisi moja ya umma huko Cameroon.
Pia amewahi kuhudumu kama waziri, mbunge na hata kuukwaa umeya.
Ili taifa lolote liweze kustawi kijamii, kisiasa na kiuchumi, ni lazima sekta ya usalama ipewe kipaumbele.
Nchi hiyo imemwachia madaraka hayo Martin Mbarga Nguélé, mwenye umri wa miaka 92, ambaye licha ya kuwa mshauri wa mambo ya usalama wa Rais wa Biya, yeye ndiye Inspekta Jenerali wa taifa hilo la Afrika ya Kati.
Ukimuacha IJP huyo, yupo Laurent Esso, ambaye ni Waziri wa Sheria wa Cameroon, akiwa na umri wa miaka 86.
Esso ameshikilia nafasi hiyo toka Disemba 9, 2011, akiwa tayari ameshaongoza wizara mbalimbali kama vile ile ya Katiba, Ulinzi, Masuala ya Umma na ile ya Mambo ya Nje.
Akiwa na umri wa miaka 86, René Claude Meka ndiye Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Cameroon.
Anashikilia moja ya nafasi kubwa ndani ya jeshi hilo.
Wakati huo huo, Baraza la Katiba nchini Cameroon linaongozwa na Clément Atangana, mwenye umri wa miaka 85.
Atangana alijiunga na Mahakama ya Cameroon kwa mara ya kwanza Disemba 20, 1968.
Hata hivyo, ameripotiwa kuwa na changamoto za afya za mara kwa mara, huku ikimlazimu kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Kama moja ya mihimili muhimu ya nchi, bunge la taifa la Cameroon linaongozwa na Cavayé Yeguié Djibril, mwenye umri wa miaka 85.
Djibril ameshikilia nafasi hiyo toka mwaka 1992.
Kwa sasa, yeye ndiye kiongozi wa chama cha Cameroon People's Democratic Movement (CPDM), akiwa mmoja ya wanasiasa wakongwe nchini humo.
Hata hivyo, taifa hilo litafanya Uchaguzi Mkuu Oktoba 5, 2025, huku Rais Paul Biya, akisisitiza nia yake ya kugombea kwa kipindi chake cha nane.