Mashabiki wa klabu ya soka ya Kituruki, Galatasaray, wameonyesha mshikamano wa nguvu kwa Wapalestina wanaokabili njaa huko Gaza, ambao wanateseka kutokana na mauaji ya halaiki na njaa iliyosababishwa na Israel. Wameunga mkono juhudi za kimataifa za "Global Sumud Flotilla," zinazolenga kuvunja mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza na kupeleka misaada ya kibinadamu.
Wakati wa mechi ya hivi karibuni, mashabiki walionyesha mabango na kuimba nyimbo za kuunga mkono msafara huo, huku ujumbe mmoja ukisisimua wengi: "Gaza, tunakuja. Fungua mpaka wa Rafah."
Msimamo huu wa mshikamano unalingana na wito unaoongezeka duniani kote wa kufunguliwa mara moja kwa mipaka na kuondolewa kwa mzingiro wa Israel, ambao umesababisha njaa kubwa Gaza.
Njaa iliyosababishwa na Israel imeua Wapalestina 332 tangu Oktoba 7, 2023, wakiwemo watoto 124. Tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la IPC (Integrated Food Security Phase Classification) litangaze rasmi njaa Gaza mnamo Agosti 22, wizara ya afya ya Gaza imerekodi vifo vya ziada 54 kutokana na njaa, wakiwemo watoto tisa.
Israel imefunga mipaka yote ya Gaza kwa misaada tangu Machi 2, na kusababisha misafara ya misaada kukwama mipakani. Kamati ya Kimataifa ya Kuvunja Mzingiro wa Gaza imesema kuwa "Global Sumud Flotilla" itaanza safari yake Jumapili kutoka Barcelona, ikifuatiwa na safari ya pili Alhamisi kutoka Tunisia, kupinga mzingiro wa Israel dhidi ya eneo la Wapalestina.
Katika taarifa, kamati hiyo ilielezea msafara huo kama maandamano ya kimataifa dhidi ya "mazingiro na mauaji ya halaiki" Gaza, huku ikiishutumu jumuiya za kimataifa kwa "kushindwa na kushirikiana."
Ilibainisha kuwa msafara huo si "boti za mfano tu zinazobeba misaada, bali ujumbe wa kibinadamu wenye nguvu" unaoonyesha azma ya kimataifa ya kumaliza mzingiro huo.
Kilio cha matumaini
"Kila meli hubeba kilio cha matumaini kwa Gaza na sauti ya kimataifa inayodai kumalizwa mara moja kwa mzingiro na dhuluma," taarifa hiyo ilisema.
Global Sumud Flotilla inajumuisha mipango minne: Maghreb Sumud Flotilla, Global Movement to Gaza, Freedom Flotilla Coalition, na Sumud Nusantara.
Waandaaji walisema juhudi hizi zinafuatia majaribio ya awali ya kupinga mzingiro huo, ikiwa ni pamoja na meli ya Kituruki Mavi Marmara mwaka 2010 na misheni za mwaka huu za meli za Al-Dhamir, Madleen, na Handala.
Vikosi vya majini vya Israel vilizuia meli ya misaada ya Handala mnamo Julai 26 ilipokaribia pwani ya Gaza na kuisindikiza hadi Bandari ya Ashdod.
Israel imeua zaidi ya Wapalestina 63,400 huko Gaza tangu Oktoba 2023.
Mwezi Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Gaza.