Wakati Morocco na DRC wanaingia uwanja wa Nyayo jijini Nairobi leo, sio tu kutafuta alama 3 za ushindi, bali lazima waweke wazi nani fahali mweupe kati yao.
Pande zote mbili ni mabingwa wa zamani, zote zikiwa zimefungana kwa pointi sita, na zote zikiwa zimebeba uzito wa matarajio kutoka kwa mashabiki wanaotaka kujua nani mwenye nguvu.
Kwa Morocco, sare itatosha kuhakikisha inafuzu kwa robo fainali.
Kwa DR Congo, Lazima wapate ushindi. Na mizani hii ndio inyofanya mechi ya Jumapili kuwa mojawapo y amechi kali zaidi zitakaandaliwa.
Simba wa Atlas wanaingia kwenye mechi wakijua wana chaguzi mbili: kushinda au sare.
Yoyote kati ya mawili hayo itawahakikishia kufuzu kwa raundi inayofuata, lakini kocha mkuu Tarek Sektioui anasisitiza kuwa yeye anataka ushindi tu.
"Hii ni mechi muhimu sana kwetu na nia yetu ni kuingia robo fainali. Ushindi ndio tu tunatafuta. Wachezaji wetu wamesalia kitaaluma, wamejitolea sana kupata ushindi dhidi ya mpinzani mgumu sana," Sektioui alisema.
Wakati Morocco iko katika fursa nzuri ya kuwa na chaguo mbili, dhamira ya DR Congo ni moja kwa moja: lazima washinde. Kocha mkuu wa Leopards Otis Ngoma anaelewa hatari inayowakumba.
"Si mechi rahisi. Hawa ni mabingwa wawili wa zamani wanakutana na kuna mengi hatarini. Zaidi ya hayo siku hii, tuna tikiti ya robo fainali ya kucheza," kocha wa DR Congo Ngoma alisema.
Pambano la Jumapili katika uga wa Nyayo Stadium sio tu wa kupima ustadi na mbinu ya mafahali hao bali pia nguvu ya kiakili na uvumilivu.
Huku vigogo wawili wa soka barani Afrika wakigongana, ni mmoja pekee ndiye atakayeibuka na uhakika wa kutinga hatua ya nane bora.