Maafisa wakuu kutoka zaidi ya nchi 30 na mashirika ya kimataifa siku ya Alhamisi walihimiza kusitishwa mara moja kuzingirwa kwa El Fasher katika jimbo la Darfur Kaskazini mwa Sudan.
Taarifa ya pamoja ilionya kuwa mamia kwa maelfu ya raia wamekwama bila chakula, maji, au huduma ya matibabu huku mapigano kati ya Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) na Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan yakiendelea.
"Pande zote kwenye mzozo zinawajibika kwa ulinzi wa raia huko Darfur na Kordofan," taarifa ya pamoja ilisema. "Hii haiwezi kuendelea," iliongeza.
Vifo na ugonjwa wa kipindupindu
Kulingana na waliotia saini, ambao ni pamoja na maafisa wakuu kutoka Uingereza, Canada, Uhispania, Norway, Uswidi, na EU, "Njia zote za biashara na za usambazaji zimekatwa, na mashirika ya kibinadamu yameshindwa kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa zaidi ya mwaka mmoja."
Walisema njaa, iliyothibitishwa kwa mara ya kwanza katika kambi karibu na El Fasher mnamo Agosti 2024, "Imeenea tangu wakati huo na inatarajiwa kuenea zaidi katika msimu wa sasa."
Zaidi ya watu 60 wameripotiwa kufariki kutokana na utapiamlo katika wiki iliyopita, huku "kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu yakizidisha athari mbaya zaidi ya utapiamlo."
Taarifa hiyo imelaani "ukiukaji wa kutisha" wa sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na "viwango vya kutisha vya unyanyasaji wa kingono vinavyohusiana na migogoro," mashambulizi kwenye masoko na hospitali, na mauaji ya watu wengi.
Uhalifu wa kivita
Ripoti hiyo ya pamoja imesema kuwa "raia zaidi ya 1,500 wameuawa" katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam mwezi Aprili, na kwamba takriban raia 40 walikufa katika shambulio la hivi karibuni kwenye kambi ya Abu Shouk.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imesema kuwa kuna kila "uhahidi unaoonyesha kuwepo kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Darfur."
Maafisa hao walitoa wito kwa RSF na washirika wake "kuacha kuizingira El Fasher," chini ya Azimio la Baraza la Usalama 2736, na "kuruhusu ufikaji wa haraka wa misaada ya kibinadamu, kwa njia salama na isio na masharti kwa watu wanaohitaji na raia kupita kwa usalama na kuondoka maeneo yenye uhasama mkali."
Pia walihimiza Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan "kufanya upya makubaliano yao ya usitishaji huu wa kibinadamu" na "kufungua kabisa kivuko cha mpaka cha Adre kwa watendaji wa kibinadamu" huku wakiondoa "vikwazo vya ukiritimba" katika utoaji wa misaada.