Baraza hilo limekataa tangazo la Kikosi cha RSF la kuunda serikali mbadala katika maeneo wanayoyadhibiti nchini Sudan, likionya kuwa hatua hiyo inatishia umoja wa taifa hilo, mipaka yake ya kitaifa, na utulivu wa kikanda.
"Tunapinga tangazo la kuundwa kwa serikali mbadala ya utawala katika maeneo yanayodhibitiwa na Kikosi cha RSF," lilisema baraza hilo siku ya Jumatano kupitia taarifa, likieleza "wasiwasi mkubwa" kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha mgawanyiko wa nchi na kuongezeka kwa janga la kibinadamu.
Lilitoa msimamo thabiti juu ya mamlaka ya Sudan, uhuru, umoja na mipaka ya kitaifa, ikisisitiza kwamba hatua za upande mmoja zinazodhoofisha kanuni hizi zinahatarisha mustakabali wa Sudan na amani katika eneo hilo.
Wajumbe walirejelea azimio nambari 2736 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi Juni, ambalo linaitaka RSF kuacha kuzingira eneo la El Fasher - mji mkuu wa Darfur Kaskazini na kitovu muhimu cha kibinadamu - na kusitisha mapigano katika maeneo yanayozunguka ambapo njaa na uhaba mkubwa wa chakula unaripotiwa.
"Wanachama wa Baraza la Usalama waliitaka RSF kuruhusu kufikiwa kwa misaada ya kibinadamu katika eneo El Fasher," ilisema taarifa hiyo, ikibainisha ripoti za mashambulizi mapya ya RSF dhidi ya jiji hilo.
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema taarifa za awali zinaonesha kuwa takriban raia 57 waliuwawa katika shambulio la Jumatatu na RSF, wakiwemo watu 40 waliokimbia makazi yao katika kambi ya Abu Shouk.
Baraza hilo pia limelaani mashambulizi ya hivi karibuni katika eneo la Kordofan nchini Sudan yaliyofanywa na pande mbalimbali, likisema yamesababisha hasara kubwa ya raia na kutatiza shughuli za kibinadamu.

Wito wa kufanywa mazungumzo
Wajumbe wa baraza hilo pia walisisitiza kwamba kuanzisha upya mazungumzo bado ni muhimu ili kusitisha mapigano, kupata usitishaji vita wa kudumu na kuandaa njia ya suluhu ya kisiasa inayohusisha wahusika wote wa kisiasa na kijamii wa Sudan.
Walizitaka pande zote kuwalinda raia, kuzingatia sheria za kimataifa na kuzingatia azimio nambari 2736, huku wakitoa wito wa kuwajibika kwa ukiukaji mkubwa.
Taarifa hiyo pia ilihimiza mataifa yote kuepuka vitendo vinavyoweza kuchochea mzozo huo na kuunga mkono juhudi za kuleta amani ya kudumu.
Kwa sasa RSF inashikilia sehemu za Kordofan Kaskazini na Magharibi, baadhi ya maeneo katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile, na majimbo manne kati ya matano ya Darfur.
Mzozo kati ya jeshi la Sudan na RSF umepamba moto tangu Aprili 2023, na kuua zaidi ya watu 20,000 na zaidi ya milioni 14 kuyahama makazi, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Utafiti kutoka chuo kikuu cha Marekani unaweka idadi ya vifo kuwa takriban 130,000.