Kwa Kenya, tayari imefuzu robo-fainali, lakini pambano la mwisho la Kundi A Jumapili dhidi ya Zambia ni zaidi ya nafasi katika nane bora.
Mechi hii wanataka kuitumia kudhibiti ubabe wao katika ardhi ya nyumbani, kuimarisha kupanda kwao chini ya Benni McCarthy, na kunyamazisha mashaka yoyote kuhusu uwezo wao wa kuwania ubingwa wa CHAN 2024.
Harambee Stars inasalia kileleni mwa Kundi A ikiwa na pointi saba, mbele ya Morocco na DR Congo, na itataka kumaliza bila kufungwa mbele ya Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi, Kasarani.
McCarthy anasisitiza kwamba wachezaji wake lazima waangalie pambano hilo kama zaidi ya utaratibu tu.
"Nawapongeza sana wachezaji, lakini sasa, tunataka kutoa tamko kwa kushinda ili mtu yeyote asiseme ni kwa bahati. Ilikuwa ni kwa bidii na uvumilivu kutoka kwa timu na kila mtu." anasema Kocha wa Harambee Stars.
Kwa Zambia, hadithi ni tofauti sana. Kushindwa mara tatu katika mechi tatu kunamaanisha kuwa Chipolopolo tayari wameondolewa, lakini kocha mkuu Avram Grant anasisitiza kuwa timu hiyo itapambana ili kumaliza kwa kasi.
"Ndio, huu ni mchezo wetu wa mwisho, kwa bahati mbaya. Lakini mashindano haya yalikuwa muhimu sana kwangu na kwa wafanyikazi wote. Ni timu mpya, na tulitaka kuona ni nani anayepatikana kwa timu ya taifa."
Mechi hii itakuwa na utofauti kutokana na adhabu iliyopewa Kenya ya utovu wa nidhamu wa mashabiki wake wakati wa mechi zilizotangulia, na sasa kamati andalizi imeppunguza idadi ya mashabiki watakao hudhuria uwanjani.
Wengine wametangaziwa maeneo ya mashabiki watakapoweza kuona mechi.
Kwa upande wa wachezaji, ari imepanda ya kushinda mechi hii baada ya Rais WIlliam Ruto kuwatangazia nyongez aya kitita cha ushindi cha shilingi milioni 2.5 iwapo watashinda mechi hii dhidi ya Zambia pamoja na nyumba kwa kikosi.