Hospitali ya Nairobi, taasisi kuu binafsi ya afya nchini Kenya, imeiomba Mahakama Kuu ya nchi hiyo kuingiliaji kati mgogoro unaoendelea katika taasisi hiyo ili kusaidia kufanya mabadiliko katika bodi yake ya uongozi.
Ombi hilo linakuja wakati ambapo, migogoro ya uongozi ya hospitali hiyo inatishia kulemaza hospitali hiyo.
Zaidi ya makampuni kumi ya bima, yamedhihirisha wazi kuwa hayatatoa tena huduma kwa wagonjwa wanaoenda katika hospitali hii.
Hospitali hiyo inathibitisha kuwa, huduma ya afya imepungua katika vituo vyake katika sehemu tofauti za jiji, huku wagonjwa wa saratani wanaofanyiwa ‘chemotherapy’ wakiwa miongoni mwa walioathirika zaidi.
Huku mipango ya matibabu ikivurugika, wengi sasa wanalazimika kubeba gharama kubwa za matibabu au kuchelewesha huduma.
“Kufuatia mkutano wa kimkakati wenye tija uliofanyika leo na watoa huduma wakuu wa bima, Hospitali ya Nairobi imekubali kusitisha utekelezaji wa mapitio yake ya bei iliyotangazwa hivi karibuni, kuanza mara moja,” Hospitali hiyo ilisema katika taarifa.
Mvutano wa uongozi
Barua mbili zinazokinzana zimeibuka kutoka Hospitali hiyo huku kila moja ikidai kuwa inatoka kwa kiongozi halali, na zote zikidai kuwakilisha bodi ya Hospitali.
Moja inatoka kwa Dkt. Barcley Onyambu na nyengine ikitoka kwa Herman Manyora, kila mmoja akisisitiza kuwa Mwenyekiti wa bodi ya usimamizi.
Katika barua hizo, Manyora anamshutumu Mkurugenzi Mtendaji Felix Osano na katibu wa kampuni Gilbert Nyamweya kwa kuongeza gharama za matibabu hadi 61% bila idhini ya bodi.
Onyambu, kwa upande wake, anapuuza uhalali wa Manyora na kumshutumu kwa ufisadi, ikiwa ni pamoja na kuomba hongo kutoka kwa watoa huduma.