AFRIKA
2 dk kusoma
Umoja wa Afrika wataka ulimwengu kutumia ramani ya dunia inayoonyesha ukubwa halisi wa Afrika
Umoja wa Afrika umeunga mkono kampeni inayolenga kukomesha matumizi ya ramani ya dunia ya karne ya 16 ya Mercator, inayotumiwa na serikali na mashirika ya kimataifa, na badala yake kutumia ramani inayowakilisha kwa usahihi zaidi ukubwa wa Afrika.
Umoja wa Afrika wataka ulimwengu kutumia ramani ya dunia inayoonyesha ukubwa halisi wa Afrika
Lengo si tu kubadilisha michoro kwenye karatasi, bali pia kuondoa kizazi kijacho kwenye mtego wa fikra potofu. / / Reuters
15 Agosti 2025

Ramani hiyo ilibuniwa na mchoraji ramani Gerardus Mercator kwa ajili ya uongozaji, lakini mchoro wake unachanganya kwa kupotosha ukubwa wa mabara: huongeza ukubwa wa maeneo karibu na ncha za dunia kama vile Amerika Kaskazini na Greenland, huku ikipunguza ukubwa wa Afrika na Amerika Kusini.

"Inaweza kuonekana kuwa ni ramani tu, lakini kiuhalisia, sivyo," naibu mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Selma Malika Haddadi aliambia Reuters, akisema Mercator ilikuza fikra potofu kwamba Afrika "ilikuwa "pembezoni", licha ya kuwa bara la pili kwa ukubwa duniani kwa eneo, likiwa na mataifa 54 na zaidi ya watu bilioni moja.

Fikra kama hizo zinaathiri vyombo vya habari, elimu na sera, alisema.

Ukosoaji wa ramani ya Mercator si jambo geni, lakini kampeni ya 'Sahihisha Ramani' (Correct the Map) inayoongozwa na vikundi vya utetezi vya Africa ‘No Filter and Speak Up' Africa’ imefufua mjadala huo, na kuyataka mashirika kupitisha makadirio ya 2018 ya Equal Earth, ambayo yanajaribu kuakisi ukubwa wa kweli wa nchi.

"Ukubwa wa sasa wa ramani ya Afrika si sahihi," Moky Makura, mkurugenzi mtendaji wa Africa No Filter, alisema.

"Ndiyo kampeni ndefu zaidi ya habari potofu na lazima ikome." Fara Ndiaye, mwanzilishi mwenza wa Speak Up Africa, alisema Mercator iliathiri utambulisho na fahari ya Waafrika, hasa watoto ambao wanaweza kukutana nayo shuleni.

"Tunafanya kazi kwa bidii katika kukuza mtaala ambapo makadirio ya ‘Equal Earth’ yatakuwa kiwango kikuu katika madarasa yote (ya Kiafrika)," Ndiaye alisema, akiongeza kuwa anatumai kuwa ndiyo itakayotumiwa na taasisi za kimataifa, zikiwemo za Afrika.

Haddadi alisema AU iliidhinisha kampeni hiyo, na kuongeza kuwa inalingana na lengo lake la "kurejesha nafasi halali ya Afrika katika jukwaa la kimataifa" huku kukiwa na ongezeko la wito wa kulipwa fidia kwa ukoloni na utumwa.

Wito wa kubadilishwa ramani

Kana kwamba hiyo haitoshi, kampeni hii ya Correct The Map, inataka mashirika makubwa duniani, kama Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa, kufuta kabisa matumizi ya Mercator.

Tayari Benki ya Dunia imeanza kutumia Equal Earth katika ramani zake rasmi, na Jumuiya ya Caribbean imejiunga katika kuunga mkono hatua hii kama ishara ya kupinga urithi wa upotoshaji wa kijiografia.

Ingawa majukwaa ya kidijitali kama Google Maps bado yanatumia mfumo wa Mercator, shinikizo la mabadiliko linaonekana kuongezeka.

CHANZO:Reuters
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us