Mfalme Charles III na Malkia Camilla wa Uingereza wamewasili nchini Kenya.
Familia ya kifalme iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) katika jiji kuu la Nairobi dakika chache kabla ya saa tano usiku, Jumatatu.
Mfalme na malkia walipokelewa na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi, ambaye ni Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri, nafasi ya juu ya uwaziri katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Balozi wa Uingereza nchini Kenya Neil Wigan alikuwepo JKIA wakati ndege ya Royal Air Force ilipotua.
Ziara ya familia ya kifalme nchini Kenya inaashiria ziara ya kwanza rasmi ya Mfalme Charles na Malkia Camilla katika taifa la Afrika, na ya kwanza kwa mwanachama wa Jumuiya ya Madola tangu kutawazwa kwao Mei 2023.
Dhuluma za kikoloni
Wanatarajiwa kukutana na familia ya kwanza ya Kenya, kuwashirikisha wafanyabiashara na wabunifu, na kuzuru mji wa pwani wa Mombasa baadaye wiki, Ikulu ya Buckingham ilisema.
Mfalme huyo pia anatazamiwa kuzungumzia suala la dhuluma za wakoloni nchini Kenya wakati wa utawala wa Waingereza.
Familia ya kifalme iko nchini Kenya kwa safari ya siku nne - kutoka Oktoba 31 hadi Novemba 3.