Mahakama ya Afrika Kusini imewahukumu kifungo cha miaka 20 gerezani raia saba wa China kwa kosa la utekaji nyara na kazi za kulazimishwa, kulingana na taarifa kutoka kwa shirika la habari la serikali.
Walithibitishwa kuwa na hatia mwanzoni mwa mwaka huu kwa utekaji nyara na kazi za kulazimishwa zinazohusisha raia 91 wa Malawi.
Hukumu hii inatokea baada ya kukamatwa kwao miaka sita iliyopita wakati polisi walipotekeleza operesheni ya kukamata watu katika kiwanda kimoja mjini Johannesburg, mji wa kibiashara, ambapo wahamiaji haramu wakiwemo watoto waliopatwa wakifanya kazi chini ya hali mbaya sana, ripoti za SABC zinasema.
Mamlaka ya Mashtaka ya Kitaifa (NPA) imepongeza hukumu hii kama hatua kubwa katika kupambana na biashara ya binadamu nchini Afrika Kusini.
“Mfumo wetu wa kusaidia waathirika wa biashara ya binadamu unaendelea,” amesema msemaji wa NPA, Phindi Mjonondwane.
Mamlaka za Afrika Kusini mara kwa mara huokoa wahamiaji wasio na hati za kusafiria, wengi wao ni wageni kutoka nchi nyingine za Afrika, ambao mara nyingi hushikiliwa na wahalifu wa biashara ya binadamu chini ya hali mbaya za kibinadamu.