AFRIKA
2 DK KUSOMA
Tanzania yakana kugeuza eneo la Isebania nchini Kenya jala la taka
Hii inafuatia madai ya afisa mazingira kutoka Kaunti ya Migori nchini Kenya kuwa baadhi ya Watanzania hutupa takataka katika mji wa  mpakani wa Isebania unaotenganisha nchi hizi mbili.
Tanzania yakana kugeuza eneo la Isebania nchini Kenya jala la taka
Kutupa taka ovyo limekuwa suala sugu katika Kaunti ya Migori. / Picha: Reuters / Others
23 Aprili 2024

Na Mustafa Abdulkadir

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Tanzania imekana tuhuma zinazowahusisha baadhi ya raia wake na madai ya utupaji wa takataka katika nchi ya jirani ya Kenya.

Kwa mujibu wa Afisa Habari katika ofisi ya Mkuu wa Mara nchini Tanzania, Rainfrida Ngatunga, hakuna taka zozote kutoka Tanzania zilizopelekwa Kenya kwa ajili ya kutupwa, kama inavyodaiwa.

"Hakuna taka yoyote iliyotupwa katika eneo la Isibania, kimsingi tumekuwa na maelewano ya muda mrefu na kwa miaka mingi sasa huku tukiadhimisha 'Mara Day' kwa pamoja," amesema Ngatunga, katika mahojiano yake na TRT Afrka.

Kulingana na Ngatunga, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara bado haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa majirani zao, kuhusiana na madai hayo.

Hapo awali, Afisa Mwandamizi wa Mazingira katika Kaunti ya Migori, Dalmas Odero, aliwaelekezea kidole cha lawama baadhi ya Watanzania kwa tuhuma za kutupa taka taka katika mji wa Isebania, Kenya.

Alisema mji wa wa Isebania ni moja wapo ya miji inayokabaliwa na changamoto za taka taka zinazotoka nchi ya jirani Tanzania. Kulingana na Odero, kuna taarifa za kuaminika za baadhi ya wakazi wa Isibania kushirikiana na baadhi ya Watanzania kutekeleza uhalifu huo.

Odero amewataka wananchi wa eneo hilo kushirikiana na mamlaka husika za usimamizi wa mazingira katika eneo hilo.

Odero pia alisema idara hiyo inafanya kazi kwa karibu na maafisa wa usalama huko Isibania kuchunguza watu wanaodaiwa kuleta taka kutoka Tanzania.

Amesisitiza kuwa, wakibainika, wahusika hao watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Pata Habari Zaidi kupitia WhatsApp channels

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us