AFRIKA
2 dk kusoma
Zimamoto yapambana kuzima moto katika msitu kaskazni mwa Morocco
Morocco imekuwa na matukio ya moto wa msituni 382 mwaka 2024, na kusababisha uharibifu wa hekta karibu 874
Zimamoto yapambana kuzima moto katika msitu kaskazni mwa Morocco
Rabat, Morocco
tokea siku moja

Mamlaka nchini Morocco zinaendelea na juhudi za kuuzima moto katika msitu kwa mkoa wa kaskazini wa Chefchaouen.

Kulingana na mwandishi wa shirika la habari la Anadolu, mamlaka zinatumia ndege kuzima moto huo, ulioanza siku ya Jumanne.

Hakuna taarifa zozote za kufariki kwa mtu kutokana na moto huo.

Moto huo ulianza katika msitu wa Dardara karibu na eneo la Chefchaouen huku viwango vya nyuzijoto vikiwa juu sana, afisa mmoja wa Shirika la Taifa la Maji na Misitu la Morocco (ANEF) amesema.

Aliongeza kuwa ndege maalum zilikuwa bado zinafanya kazi kuuzima moto huo.

“Watu katika eneo hilo hawakulala usiku kucha wakiwa wanafanya kazi kuuzima moto huo,” Suleiman Rakib, mkazi mmoja, aliliambia Anadolu.

Aliongeza kuwa moto huo umesababisha hasara kubwa, hasa kwa miti ya mizeituni.

Kulingana na walioshuhudia, maeneo ya misitu yenye milima yamefanya iwe vigumu kwa wazimamoto kudhibiti moto.

Siku ya Jumatatu, Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Morocco imeonya kuwepo kwa joto kali hadi viwango vya nyuzijoto 46°C (114.8°F) katika maeneo kadhaa, na kutarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa.

Mamlaka nchini Morocco yalieleza kuwepo kwa matukio 382 ya moto wa msituni 2024, na kusababisha uharibifu wa karibu hekari 874 – ikiwa ni upungufu wa asilimia 82 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Misitu nchini Morocco ni asilimia 12 ya ardhi ya nchi hiyo, na nchi hiyo inakabiliwa na matukio mabaya kila mwaka kutokana na hali ya hewa na shughuli za watu.

CHANZO:AA
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us