AFRIKA
2 dk kusoma
Rwanda kuhesabu ndege aina ya korongo wa majivu
Mwaka wa 2024, Rwanda ilikuwa na jumla ya korongo wa kijivu 1,293.
Rwanda kuhesabu ndege aina ya korongo wa majivu
Korongo wa kijivu ni ndege ambaye anatambulika kwa urembo wake/Picha: Getty / Getty Images
12 Agosti 2025

Serikali ya Rwanda imeanza mchakato wa kuwahesabu korongo wa kijivu, yaani grey crested crane.

“Timu yetu itaanza kazi hii kwa siku 3 kwa ajili ya sensa ya 9 ya kila mwaka ya ndege hawa mashuhuri,” Shirika la Uhifadhi la Wanyamapori la Rwanda, RWS limesema katika taarifa mtandaoni.

“Kwa miaka mingi, tumejivunia ongezeko la mara kwa mara la idadi yao - na tunatumai wameongezeka mwaka huu,” imesema taarifa hiyo.

Korongo wa kijivu ni ndege ambaye anatambulika kwa urembo wake. 

Mwili wake wa kijivu unatofautiana sana na mabawa yake meusi na meupe, na pochi nyekundu inayong'aa kwenye koo. 

Jambo la kuvutia zaidi, manyoya ya dhahabu hutengeza taji linalozunguka katika vichwa vyao. 

Mbali na Rwanda, ndege hao pia wanapatikana kwa wingi nchini Uganda na hata kutambulika kama ndege wa taifa wa nchi hiyo.

Korongo wa kijivu pia wanapatikana Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Msumbiji, Afrika Kusini na Zimbabwe.

“Kama sehemu ya mtandao wetu wa ushirikiano wa kuvuka mpaka, pia tunafanya kazi pamoja na timu kutoka Uganda, Tanzania, na Burundi kuhesabu korongo katika maeneo ya mpaka wa pamoja. Kwa pamoja, tunatoa picha kubwa zaidi ya hali ya spishi hiyo kote Afrika Mashariki,” Shirika la Uhifadhi la Wanyamapori la Rwanda limesema.

Mwaka wa 2024, Rwanda ilipata idadi ya korongo wa kijivu 1,293 nchini humo.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us