AFRIKA
2 DK KUSOMA
Msumbiji: Vifo vinavyotokana na matokeo ya uchaguzi vyafikia 27
Nchi hiyo ilishuhudia machafuko makubwa siku ya Alhamisi, huku waandamanaji wakipinga ushindi wa chama cha Frelimo ambacho kimekuwa madarakani toka mwaka 1975.
Msumbiji: Vifo vinavyotokana na matokeo ya uchaguzi vyafikia 27
Msumbiji inakabaliwa na vurugu baada ya uchaguzi wa Oktoba 9, 2024./Picha: Reuters   / Others
8 Novemba 2024

Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia vurugu za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji sasa imefikia 27, kufuatiwa kuuwawa kwa waandamanaji watatu siku ya Alhamisi, maofisa wa afya nchini humo wamesema.

Hayo yanajiri huku mamlaka nchini humo, ikipeleka askari kwenye maeneo mbalimbali kudhibiti hali ya usalama nchini humo.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Msumbiji, Jenerali Omar Msaranga jeshi hilo lipo tayari kuwasaidia polisi kurejesha utulivu nchiini Msumbiji.

Maandamano yenye vurugu

Miji mingi nchini Msumbiji imeghubikwa na vurugu na maandamano ya mara kwa mara, toka Tume ya Uchaguzi nchini humo (CNE) kumtangaza Daniel Chapo kutoka chama cha Frelimo kama mshindi wa kiti cha Urais dhidi ya Venancio Mondlane kutoka chama cha upinzani.

Kwa upande wake, Mondlane ameitisha mgomo wa wiki nzima ulioanza Oktoba 31, wenye kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Mamia ya waandamanaji walifurika kwenye mitaa ya jiji la Maputo siku ya Alhamisi, kuitikia wito wa Mondlane.

Chama cha Frelimo kimekuwepo madarakani toka nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wareno, mwaka 1975.

Tuhuma za wizi wa kura

Vyama vya upinzani vimekituhumu chama cha Frelimo kwa udanganyifu kwenye uchaguzi wa Oktoba 9, huku wasimamizi wa kimataifa wakitilia dosari mchakato huo.

Chama cha Frelimo kimekuwa kikituhumiwa kwa wizi wa kura nchini humo. Hata hivyo, Baraza la Katiba la nchi hiyo, bado halijaidhinisha matokeo ya uchaguzi huo kama inavyopaswa kufanyika.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us