Mahakama ya juu kabisa nchini Afrika Kusini imeamuru kuwa wanaume wanaweza kuchukua majina ya ukoo ya wake zao, uamuzi ambao umepongezwa kama hatua inayowaleta wanaume na wanawake kwenye usawa wa kisheria katika ndoa.
Mahakama hiyo ilitangaza kuwa kipengele cha Sheria ya Usajili wa Kuzaliwa na Vifo, ambacho kilishurutisha wanaume kuomba kibali kutoka kwa mamlaka kabla ya kubadilisha jina lao, huku wanawake wakipata haki hiyo moja kwa moja baada ya ndoa, talaka au kifo cha mume, ni kinyume cha katiba.
Katika uamuzi huo uliotolewa siku ya Alhamisi, mahakama iligundua kuwa hili ni ubaguzi wa kijinsia usio wa haki kwa sababu haliwapi wanaume haki sawa za moja kwa moja, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la SABC.
“Mahakama ilibaini kuwa kushindwa kwa wanaume kuchukua majina ya wake zao ni aina ya ubaguzi,” mahakama ilisema katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii.
Ruhusa imekataliwa
Kesi hii ilifikishwa mbele ya mahakama na wanandoa wawili - Jana Jordaan na Henry Van Der Merwe, pamoja na Jess Donnelly-Bornman na Andreas Nicolas Bornman.
Van Der Merwe alisema hakupewa ruhusa ya kuchukua jina la mke wake, naye Bornman alisema alikataa alinyimwa haki ya kuunganisha jina lake na la mke wake.
"Wawili hao walikuwa wamefanikiwa kupinga kifungu hicho mahakama kuu, lakini bado walihitaji Mahakama ya Juu kabisa kuthibitisha kuwa kifungu hicho ni batili kikatiba ili hatua hiyo iweze kuanza kutekelezwa," SABC imeripoti.
Mahakama ya Katiba ilisema kuwa kifungu hicho kiliwanyima wanawake "haki ya kutumia jina lao la ukoo kama jina la familia pale ambapo waume zao wanataka kutumia jina hilo."