Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, ameibuka mshindi katika kesi aliyoifungua kupinga kuenguliwa kwenye mchakato wa urejeshaji wa fomu za uteuzi wa kugombea urais.
Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia jopo la majaji watatu, imeamuru mchakato huo uendelee kutoka pale uliposimama.
Uamuzi huo umetolewa leo jijini Dodoma na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu likiongozwa na Majaji Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza.
Kesi hiyo, iliyofunguliwa kwa hati ya dharura na bodi ya wadhamini wa ACT-Wazalendo pamoja na Mgombea huyo wa Urais, ilipinga uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wa kumzuia Mpina kurejesha fomu za uteuzi, hatua iliyokuwa ikimwondoa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, Mpina sasa anaruhusiwa kuendelea na mchakato wa kugombea urais, hatua inayofanya jumla ya vyama vitakavyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania kufikia 18.
Uchaguzi nchini Tanzania unategemea kufanyika Oktoba, 29, 2025.