Wanaingia kwenye uwanja wa Moi Kasarani Agosti 30 kama mabingwa mara mbili wa michuano ya CHAN, wakiwa wametwaa ndoo hiyo mwaka 2018 na 2020.
Kwa taarifa yako tu, Morocco wanashika nafasi ya 12 kwa ubora wa soka duniani, na nafasi ya kwanza barani Afrika, wakidhihirisha ubabe wao wa kusakata kabumbu.
Morocco ndiyo timu anayotokea beki namba mbili ya PSG, Achraf Hakimi na super sub wa Real Madrid, Brahim Diaz.
Katika safari yao ya CHAN, Morocco walianza kwa kuifunga Angola bao 2-0 kabla ya kuduwazwa na Harambee Stars kwa kukubali nyavu yao kutikiswa mara moja bila majibu.
Wakafufua matumaini walipowazaba Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kufanikiwa kumaliza wa pili kwenye kundi A.
Kwa hatua hiyo ikawalazimu kukwaa pipa hadi bongo, kukabiliana na vijana wa Rais Samia Suluhu Hassan katika mchezo wa robo fainali.
Huko waliacha kilio na kukata kamdomo ka mashabiki wa Taifa Stars kwa kuwachapa bao 1-0 kabla ya kuwafungisha virago mabingwa wengine wa mara mbili wa michuano hayo, Senegal au Simba wa Teranga, katika hatua ya nusu fainali.
Simba kutoka Milima Atlas wanarejea katika hatua waliyoizoea, ila siku zote unakumbushwa badilika usiishi kwa mazoea.
Simba huyu atakubali kuchezewa sharubu zake na Ng’ombe wa Madagascar?