Omar Abdulkadir Artan ameweka historia kwa kuwa mwamuzi wa kwanza wa Kisomali kuchaguliwa kushiriki kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA.
Yeye ni miongoni mwa waamuzi watatu wa kati waliochaguliwa kutoka Afrika na mwakilishi pekee kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara atakayehudumu katika Kombe la Dunia la FIFA U-20 mwaka 2025.
Mashindano hayo ya kimataifa ya soka yamepangwa kufanyika kuanzia tarehe 27 Septemba hadi 19 Oktoba nchini Chile.
Artan atajiunga na Jalal Jayed wa Morocco na Youcef Gamouh wa Algeria kama waamuzi wakuu kutoka bara la Afrika.
Akiwa ni mwanzilishi katika soka la Kisomali, Artan hapo awali alikua mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kusimamia fainali ya bara, akisimamia ushindi wa Pyramids FC ya Misri dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini jijini Cairo. Pia amewahi kuhudumu katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Waamuzi wasaidizi wengine waliochaguliwa kutoka Afrika ni pamoja na Gilbert Cheruiyot (Kenya), Abelmiro Montenegro (São Tomé na Príncipe), Khalil Hassani (Tunisia), Eric Ayimavo (Benin), Lahsen Azgaou (Morocco), na Mostafa Akarkad (Morocco).